Mazao ya Wanyama kuongezeka zaidi ya mara mbili ifikapo mwaka 2020


Naibu Waziri wa Mifugo, Abdallah Ulega amesema takwimu kutoka Shirika la Chakula Duniani (FAO) zinaonesha kuwa mwanzo wa milenia hii mahitaji  ya mazao ya wanyama yalikadiriwa kuongezeka zaidi ya mara mbili ifikapo mwaka 2020 ambapo mwelekeo huu wa ulaji wa mazao ya wanyama umeitwa – Mapinduzi katika Ufugaji wa Wanyama.

Matokeo ya utafiti wa kitaifa uliofanyika mwaka 2012/13 pia yalionesha kuwa kaya nyingi zinatemea wanyama kwa ajili ya kujikimu kimaisha na shuguli za maendeleo ya kiuchumi, ambapo wanyama wamekuwa ni vyanzo vya moja kwa moja vya vyakula kama vile nyama, maziwa, na mayai. Pia wanyama kazi ni nyenzo muhimu katika uzalishaji wa mazao wa moja kwa moja katika kilimo kutokana na wanyama hao kutoa mboji inayotumika katika kilimo na uzalishaji wa gesi asilia kwa ajili ya kuzalisha umeme au kupikia na hivyo kuzuia au kupunguza kabisa tatizo la uharibifu wa mazingira.

Hayo yamesemwa na Ulega wakati akifungua Mdahalo juu ya vyakula vya asili ya wanyama na mchango wake katika masuala ya afya ya umma na lishe, na uzinduzi wa mikakati ya kitaifa ya kuzuia na kudhibti magonjwa ya brusela na kimeta kwa binadamu na wanyama katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Afya Muhimbili MUHAS jana jijini Dar es salaam.

Katika ripoti ya Benki ya Dunia inaonesha kuwa nchini Tanzania miongoni mwa kaya zenye mafanikio zaidi huko vijijini na ambazo  zipo katika hatua za kuuaga umaskini, ni zile ambazo zimechanganya shughuli zake na kujumuisha ufugaji.

Ulega ameongeza kuwa Vile vile, Tanzania inashikilia nafasi muhimu ya mafanikio ya kujitosheleza katika mahitaji ya vyakula kwa Bara la Afrika ifikapo mwaka 2050.

Ni wazi kuwa, Kauli Mbiu ya Siku ya Chakula Duniani ya Mwaka Huu “Lishe Bora Kwa Ulimwengu Usio na Njaa” ina maanisha dira ya kuhakikisha kuwa wanyama tuwafugao tunawatumia vyema katika kuchangia kwenye uhakika wa kupata chakula na lishe bora pamoja na usalama wa chakula mbali ya mambo mengine.

Waziri Ulega amesema hivi karibuni Wizara imeanza programu za kudhibiti magonjwa nchi nzima ili kuongeza viwango na ubora wa vyakula vitokanavyo na wanyama.