https://monetag.com/?ref_id=TTIb RC Dodoma atoa agizo kwa Maofisa mipango Miji 'Msisubiri kuvunja majengo ya watu' | Muungwana BLOG

RC Dodoma atoa agizo kwa Maofisa mipango Miji 'Msisubiri kuvunja majengo ya watu'


Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge amewaagiza maofisa mipango miji na wapima ardhi kutumia ujuzi na utaalamu wao kulisaidia taifa, badala ya kusubiri majengo yasimame ndipo wawavunjie watu.

Dk. Mahenge alitoa kauli hiyo jana wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa maofisa mipango miji na wataalamu wa ardhi yaliyoratibiwa na Shirika la African Institution For Capacity Development (AICARD) na kushirikisha wataalamu hao kutoka mikoa ya Singida, Morogoro, Iringa na Dodoma.

Katika hotuba ya Dk Mahenge iliyosomwa na Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Jabir Shekimweri, alisema wataalamu hao wanatakiwa kufanya kazi kwa umakini mkubwa kwa kuwa miji mingi inakuwa kwa kasi kutokana na ongezeko la watu. Aliwataka kuongeza kasi ya kupanga miji katika maeneo yote na isiwe mijini pekee kwani hata vijijini kuna ongezeko kubwa la ujenzi wa majengo kutokana na miundombinu kuboreshwa ikiwemo umeme wa Wakala wa Umeme Vijijini(REA).

"Ongezeni kasi ya kupanga miji, watu wamekuza uchumi na wanataka kujenga majengo mazuri, wanashindwa kutokana na kutopangwa kwa miji na hata wakijenga hayana mpangilio mzuri na matokeo yake baadaye wanakuja kuvunjiwa kwa kuambiwa hawajajenga panapostahili," alisema.

Aliyataka mashirika yanayotoa elimu kuwashirikisha wenye mamlaka katika halmashauri wakiwemo wakurugenzi kwani ndiyo wenye maamuzi. Alisema lengo la kufanya hivyo ni kuondoa migongano inayotokea kwenye halmashauri kwa kutoelewana kwa wakurugenzi.