Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Loata Ole Sanare amewatoa hofu wananchi wa Mkoa huo huku akiwahakikishia kuwa yeye ameteuliwa na Mhe. Rais Dkt John Pombe Magufuli kuwa kiongozi wa wananchi wote na kwamba kitakachozingatiwa katika utendaji wake wa kazi ni, Kanuni, sheria taratibu na miongozo iliyopo.
Sanare ametoa kauli hiyo akiwa katika ziara ya kujitambulisha rasmi katika Wilaya zote saba (7) zenye Halmashauri Tisa (9) za Mkoa wa Morogoro, Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa ikiwa ni halmashauri ya pili kwenda kujitambulisha baada ya hivi karibuni kujitambulisha Katika Halmashauri ya Wilaya ya Gairo.
Akiwa Wilayani Kilosa, Sanare amezungumza na makundi mbalimbali ya Halmashauri hiyo ikiwa ni pamoja na kundi la Watumishi wa Halmashauri hiyo, Wakuu wa Idara na Taasisi za Serikali ndani ya Wilaya ya Kilosa pamoja na Kundi la jamii ya wakulima na wafugaji.
Akiongea na viongozi kutoka Kundi la Jamii ya Wakulima na Wafugaji, Mhe Sanare amewataka wanamorogoro kuondoa hofu kuhusu utendaji kazi wake na kwamba yeye kutoka jamii ya wafugaji hakumzuii kutekeleza majukumu yake kwa usawa.
“Ni kweli mimi ni mfugaji, lakini ni mfugaji niliyetumwa kuja kufanya kazi na wafugaji wenzangu kwamba kuna sheria za nchi na taratibu, tuzifuate. Ni mfugaji niliyetumwa kuja kuwaambia wakulima tuangalie na haki za wafugaji, na ninyi upande huu tuangalie na haki za upande wa pili…kwamba Mkuu wa Mkoa aliyekuja si Mkuu wa Mkoa wa Wafugaji ni Mkuu wa Mkoa wa makundi yote yaliyopo, ” alisisitiza Sanare.
Kuhusu kukomesha migogoro ya Ardhi amesema migogoro hiyo pamoja na sababu nyingine kwa kiasi kikubwa inasababishwa na watendaji wa Serikali katika ngazi za chini wakiwemo Watendaji wa Vitongoji, Watendaji wa Vijiji, Kata, Tarafa pamoja na Wenyeviti wa Vijiji.
Kwa sababu hiyo amewataka watendaji hao kujirekebisha, kubadilika na kuchukua hatua kwa kuwa kuanzia sasa mgogoro wowote wa Ardhi utakapotokea mtu wa kwanza atakayehojiwa na ikibidi kuchukuliwa hatua ni Watendaji wote waliotajwa hapo juu.
Katika Hatua nyingine akiongea na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Mhe. Sanare amemwagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo pamoja na Viongozi wa Halmashauri ya Kilosa kuwarejesha mara moja watumishi wa Idara ya
Uhasibu wanaotuhumiwa kwa ubadhilifu wa fedha za Umma zaidi ya Tsh. 700Mil. ili waweze kujibu tuhuma zinazowakabili.
Mkuu huyo wa Mkoa kupitia hadhara hiyo aliwahimiza Wananchi wa Wilaya ya Kilosa kujiandiskisha kwenye daftari la wapiga kura ili kupata haki zao za msingi za kupiga kura katika uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 24 mwaka huu, huku akiwataka wananchi wakati ukifika wamchague kiongozi mchapa kazi na mwenye hofu ya Mungu.
