Wananchi tembeleeni maonesho kujua Elimu ya lishe bora- RC Singida


Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi ametembelea mabanda ya maonesho kwenye Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani  yanayofanyika Kitaifa katika uwanja wa Bombardier,Manispaa ya Singida.

Amesema uwepo wa maadhimisho haya ni fursa kwa wananchi wote kutambua umuhimu wa lishe bora kwa afya.

Amebainisha kuwa elimu juu ya uandaaji chakula tangu kikiwa shambani,baada ya mavuno,wakati wa kukiandaa nyumbani na wakati wa kupika inatakiwa ili mwananchi ale mlo kamili na bora.

Dkt. Nchimbi amewasihi wataalam wa lishe nchini kutoa elimu sahihi kwa wananchi kuelewa makundi  muhimu ya chakula kinachopaswa kutumiwa na binadamu.

“Uwepo wa maadhimisho haya ya kitaifa Singida usaidie jamii kutambua umuhimu wa lishe bora kwa ustawi wa afya za watu ili washiriki kikamilifu katika ujenzi wa taifa,” alisema Nchimbi.

Aidha, Mkuu huyo wa mkoa amewasihi wananchi kujitokeza kwa wingi kupata elimu juu ya lishe bora na teknolojia rahisi ya kuongeza thamani ya mazao ya chakula.

Uzinduzi rasmi wa maadhimisho hayo utafanyika Jumapili ijayo na yatahitimishwa tarehe 16 mwezi huu.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni ” Lishe Bora kwa Ulimwengu Usio na Njaa”.