RC Pwani aelekeza usajili watoto chini ya miaka mitano kuvuka asilimia 90


Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo ametoa maelekezo kwa viongozi mkoani hapa kuhakikisha kuwa usajili na utoaji wa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto waliochini ya miaka mitano unafikia Zaidi ya asilimia 90 ndani ya miezi mitatu kuanzia sasa.

Akifungua semina kwa viongozi wa Mkoa na wilaya juu ya Mpango wa usajili wa watoto walio na umri chini ya miaka mitano iliyofanyika Wilayani Mkuranga, Mhandisi Ndikilo alisema kuwa takwimu zinaonesha kuwa kwa sasa waliosajiliwa na kupewa vyeti vya kuzaliwa mkoani Pwani ni asilimia 14.5 tu, hivyo akawaeleza viongozi hao kuwa wanao wajibu wa kuhakikisha kuwa zoezi hilo linaratibiwa vizuri ili kufikia lengo la kusajili na kutoa vyeti kwa watoto wote walio na vigezo.

Akifafanua jukumu la kila mdau, Mhandisi Ndikilo aliwaasa wakurugenzi na timu zao kwenda kutekeleza kwa ufanisi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wananchi wanapata elimu ya kutosha kuhusu jambo hili na wakuu wa wilaya kufanya ufuatiliaji wa karibu.

“Halmashauri wanapewa fedha za utekelezaji wa mpango huu, ninawaasa zikatumike kwa matumizi yaliyokusudiwa na si vinginevyo, madiwani wasiwakomalie wakurugenzi kutumia fedha hizo, kazitumieni vizuri ili mfanye kazi hii sawasawa, msije mkaiona fedha hiyo kuwa ni yenu” alisisitiza Mhandisi Ndikilo.

Mhandisi Ndikilo alieleza kuwa Mpango huu utasaidi kuondoa tatizo la kuchelewa kwa upatikanaji wa Vyeti vya kuzaliwa kwa Wananchi wa Mkoa Pwani kwa kuwa limepatiwa suluhisho la kudumu na akatahadharisha kuwa wasajili katika vituo waondoe urasimu wakati wa usajili na kutoa vyeti kwani huduma hiyo inatekelezwa bila malipo yoyote kutoka kwa mzazi au mlezi wa mtoto husika, hivyo wasiitumie kama moja ya njia ya kujipatia kipato.

Awali katika katika taarifa yake Kaimu Mkuu ambaye ni Afisa Mtendaji wa RITA Bi. Emmy Hudson alieleza kuwa hadi sasa kupitia mpango huo utekelezaji katika mikoa 15 umesaidia kuwapatia hati watoto bila kujali hali zao na kupandisha takwimu kutoka asilimia 13 mwaka 2012 hadi 49 mwaka 2019.

Bi. Hudson aliongeza kuwa miongoni mwa mambo mengine, Mpango huo umesaidia pia upatikanaji wa (papo kwa hapo) haraka wa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wanaozaliwa pamoja na upatikanaji wa takwimu zilizo sahihi.