Vijiji 8,102 vyapata umeme


Katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais John Magufuli, serikali imeongeza kasi ya kusambaza umeme vijijini, ambapo vijiji 8,102 vimekwisha fikiwa na nishati hiyo.

Hayo yamebainishwa jijini Dodoma na Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Leonard Masanja alipozungumza na gazeti hili kuhusu mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha utawala wa Rais Magufuli.

Masanja alisema hadi kufikia Oktoba mwaka huu, serikali imefanikiwa kupeleka umeme katika vijiji 8,102 vya Tanzania Bara, ikilinganishwa na vijiji 2,018 vilivyokuwa vimeunganishwa umeme mwaka 2015.

"Hii ni sawa na ongezeko la vijiji 6,084 katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita ambayo ni asilimia 301," alisema Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu.

Kwa miaka mitatu ya utekelezaji miradi ya kupeleka umeme vijijini, serikali imetumia zaidi ya Sh bilioni 968.861, zote zikiwa ni fedha za ndani.

Akifafanua, Masanja alisema “Kwa mwaka 2016/17 serikali ilitumia shilingi 316,472,081,063, mwaka 2017/18 shilingi 333,528,113,624 na mwaka 2018/19 shilingi 318,861,767,811 ambazo zote ni fedha za ndani na kodi za wananchi.

Aidha, Masanja alisema katika kipindi cha utawala wa Rais Magufuli, serikali imekamilisha Mradi wa Ujazilizi Mzunguko wa Kwanza (Densification Round One), uliotekelezwa katika mikoa nane ya Arusha, Iringa, Mara, Mbeya, Njombe, Pwani, Songwe na Tanga.

"Kupitia mradi huu, miundombinu ya kusambaza umeme imekamilika kwa asilima 100. Hadi kufikia mwezi Juni mwaka huu, vijiji vyote 295 vilivyokuwa katika wigo wa mradi vimeunganishwa umeme," alisema.

Utekelezaji wa mradi wa ujazilizi mzunguko wa pili, utahusisha kuongeza wigo wa kuunganisha umeme katika vitongoji vilivyobaki (vilivyorukwa); hivyo kuwezesha wananchi wengi zaidi kufikiwa na umeme.

Kazi hiyo imepangwa kufanyika katika mwaka wa fedha wa 2019/2020. Ifikapo Juni mwakani vijiji zaidi ya 10,278, kati ya vijiji 12,268 vya Tanzania Bara, vitaunganishwa umeme sawa na asilimia 84 ya vijiji vyote nchini.

Hotuba ya bajeti ya mwaka 2019/2020, iliyosomwa bungeni mjini Dodoma na Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani, inaonesha kuwa hadi Mei mwaka huu wilaya na halmashauri 15 zilikuwa zimeshafikishiwa umeme katika vijiji vyake vyote na kazi inayoendelea ni kuunganisha umeme katika vitongoji vyake.

Wilaya na halmashauri hizo ni Mafia, Bahi, Siha, Moshi, Hai, Mwanga, Rombo, Madaba, Buhigwe, Makambako, Korogwe Mjini na Mafinga. Kwa mwaka wa fedha 2019/2020, serikali imetenga Sh bilioni 363.11 za kutekeleza Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu.