Frederick Sumaye atangaza kuhama CHADEMA


Waziri mkuu mstaafu wa Tanzania, Frederick Sumaye ametangaza kuondoka ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na kusema kwa sasa atakaa bila chama.

Ametangaza uamuzi huo leo katika mkutano wake na waandishi wa habari ambapo amedai kujiunga upinzani si jambo rahisi, kwamba alikuwa akiandamwa na Dola pamoja na familia yake.

"Mimi siyo mwanachama wa Chadema kuanzia sasa na sijiungi na chama kingine cha Siasa kuanzia leo na niko tayari kutumika katika chama chochote hata Chadema katika kushauri" - Frederick Sumaye

Sumaye aliyekuwa waziri mkuu mwaka 1995 hadi 2005 amesema hayo takribani siku nne tangu alipopigiwa kura 48 za hapana kati ya 76 katika uchaguzi wa uenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani.

Kuhusu kugombea nafasi ya Uenyekiti ndani ya CHADEMA, amesema, "Leo natangaza kuwa hiyo safari ya kugombea uenyekiti wa ngazi ya taifa naisitisha leo, kwa usalama wangu na familia kwa ujumla na Mbowe aliwahi kunitahadharisha kuwa sumu haionjwi kwa ulimi namimi sitaki kuionja".