Prof. Mbarawa aiagiza bodi mpya ya RUWASA kwenda kumaliza tatizo la maji Vijijini



Na Ezekiel Mtonyole, Dodoma.

Waziri wa Maji Profesa Makame Mbarawa imeitaka bodi mpya ya mamlaka ya Maji Safi na usafi wa Mazingira vijijini RUWASA kuhakikisha inakwenda kuondoa changamoto zilizopo ndani ya Mamlaka hiyo ili kuhakikisha malengo ya Serikali ya kuanzisha Wakala huo inakamilika na wananchi wa vijijini wanapata huduma ya maji Safi.

Wakati wa kuzindua bodi hiyo mpya Waziri  Mbarawa amesema Wakala huo umeundwa ili kuondoa changamoto zote zilizopo katika Mamlaka hiyo na kuhakikisha malengo ya yanatimia ya kuhakikisha wananchi hasa wa vijijini wanapata huduma ya maji Safi.

"Tatizo la huduma ya maji Safi  vijijini ni kubwa niwape changamoto bodi mpya mkahakikishe changamoto hizo zinatatuliwa hasa tatizo la miradi mingi kutokamilika kwa wakati" amesema.

Profesa Mbarawa amesema kumekuwa na madudu mengi ambayo yakifanywa na watendaji katika utendaji wao wa kila siku jambo ambalo halikubaliki kabisa.

Amesema uzinduzi wa bodi hii ukawe chachu ya kuifanya RUWASA iwe mfano wa kuigwa na bodi nyingine katika utendaji kazi zao za kila siku.

"Naamini bodi hii itakwenda kufanya mabadiliko makubwa na ndio bodi ya kwanza kuzinduliwa katika Mamlaka hii, "amesema.

Kuhusu kuanza kutumia force acaunt kwa baadhi ya miradi  amesema imeanza kuleta matokeo mazuri kwani Kuna miradi imejengwa kwa fedha ndogo tofauti na wangetumia wakandarasi kitekeleza miradi hiyo.

"Watu hawaipendi force account kwasababu ya maslahi yao binafsi hivyo basi mwelekeo wa Wizara tutaanza kutumia kwenye miradi mingi kwani umeonyesha mafanikio. amesema.

Naye Naibu Waziri wa Maji Jumaa Aweso amesema wataalamu wanapaswa kuelekeza nguvu zao vijijini ili kutatua changamoto za maji zilizopo  katika sekta ya maji.

Amesema watu wa vijijini wamekuwa wakipata shida ya maji na kunywa maji wanayokunywa ambayo pia hutumiwa na wanyama.

"Naomba wataalamu mtumie ujuzi mliopata ili kuokoa tatizo la maji hatupendi kusikia kila kukicha shida ya maji,"amesema Aweso.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa bodi ya RUWASA profesa Idriss Mshoro amesema bodi yao iko tayari kutekeleza kile walichoagizwa ili jamii iweze kupata maji.

Amesema anashkuru Rais Dk John Magufuli kwa kumteua katika nafasi hiyo ambayo amesema ataitendea haki.

Wakati  Katibu wa Wizara ya Maji Profesa Kitila Mkumbo amesema wameanzisha mamlaka hiyo ili kutatua changamoto za maji vijijini hivyo watendaji wanapaswa kuwajibika.