Elimu kwa Wananchi juu ya vipimo sahihi katika bidhaa bado ni tatizo kubwa



Na John Walter-Babati-Manyara

Imebainika kuwa ukosefu wa elimu kwa wananchi kuhusiana na matumizi sahihi ya vipimo vya  uzito, ujazo, urefu na ufungashaji wa bidhaa kwenye viwanda kumesababisha walaji kukosa haki zao za kupata bidhaa kulingana na fedha halisi wanazonunua mahitaji.

Meneja wa Wakala wa Vipimo Mkoani Manyara Wakili Mosses Mbunda amesema kuwa  kazi kubwa ya wakala wa vipimo ni kumlinda  mlaji  katika sekta za biashara, Afya, Usalama na Mazingira kupitia  matumizi ya vipimo sahihi.

Amesema kuwa wananchi wamekuwa wakiibiwa kutokana na kukosa elimu ya matumizi sahihi ya vipimo ikiwemo kipimo cha mizani ambacho hutumika zaidi katika mabucha, upimaji wa sukari na vipimo vya mafuta ya kupikia.

Amesema jukumu lingine ni kuilinda jamii kuepukana na madhara yatokanayo  na matumizi  mabaya  ya vipimo  katika sekta za biashara, Afya, Usalama na Mazingira ikiwa ni utekelezaji wa sheria  na kanuni kwa kusimamia matumizi sahihi ya vipimo Mkoani humo.

“Usimamizi wa sheria na kanuni ni pamoja na kutembelea vituo na taasisi zilizoko Wilayani ili kuhakikisha vipimo vya ujazo, urefu na uzito vinapitiwa, kwenye vipimo vya uzito vya mizani  maduka, masoko”,

“Vipimo vingine katika hospitali, klinik vya kupimia watoto wadogo  na wagonjwa  ili daktari aweze kutoa matibabu sahihi ambapo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara  tayari vipimo vimekaguliwa, vituo vya Afya vya watu binafsi  na tuna mpango wa kuzifikia hospitali za Dareda na Haydom” Alisema Mbunda.

Alivitaja vipimo vingine kuwa ni ufungashaji  wa bidhaa  katika viwanda mbalimbali katika kuangalia ujazo unaokidhi ubora na kutoa ushauri jinsi ya kuboresha vifungashio ikiwa ni pamoja na kupima madini katika soko la madini  katika Halmashauri husika.

Kuwa kiungo kati ya Taifa  na Taasisi  za kikanda na kimataifa katika masuala ya vipimo pamoja na kutoa ushauri  wa kitaalamu kuhusu masuala ya Vipimo kwa wadau.

Kuhakikisha vifaa vyote vitumikavyo Nchini kama standards za vipimo  vinaulinganisho sahihi na ule wa Kimataifa.

Ameeleza kuwa kupitia kamati ya ushauri ya Mkoa  wanajukumu la kuhamasisha matumizi sahihi ya vipimo vya mazao na kuhamasisha wakurugenzi kutenga maeneo ya vituo maalumu vya ukaguzi wa mazao na si kutumia rumbesa inayowakandamiza wakulima.

Musa Hassani mkazi wa Babati  alisema kuwa Wakala wa vipimo mkoani humo imesaidia kuongezeka kwa vipimo vinavyokaguliwa mara kwa mara hata katika ukaguzi wa mitungi ya gesi ya kupikia ambapo awali mitungi hiyo ilikuwa haipimwi ujazo wake na kuwapunja wateja.

“Hii inalinda haki katika biashara, nanunua bidhaa yenye ujazo, uzito,  na  urefu kulingana na fedha ninayoitoa pia Napata ushauri wa kitaalamu kuhusu masuala ya vipimo” Alisema.

Mpya zaidi Nzee zaidi