Naibu Waziri Mgalu asaini makubaliano Sekta ya Nishati Baraza la Mawaziri EAC

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, amesaini makubaliano ya Sekta ya Nishati ya mkutano wa Baraza na Mawaziri wa Afrika Mashariki kwa niaba ya Waziri ya Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani.

Mkutano huo umefanyika Januari 14, 2019, ambapo kila nchi huufanya nchini kwake, hapa nchini mkutano huo umefanyika jijini Dodoma kwa kushirikisha Viongozi Waandamizi wa Wizara ya Nishati, Mashirika pamoja na Wakuu wa Taasisi zilizochini ya Wizara hiyo.


Majadiliano ya Mkutano huo huendeshwa kwa njia ya mtandao (Video Conference) kwa kuwakutanisha Mawaziri wa sekta husika kutoka nchi zote wanachama.


Mkutano huo hujadili taarifa mbalimbali iliyowasilishwa kwao na Makatibu Wakuu wa Wizara husika katika sekta hiyo zinayohusu miradi mbalimbali ya maendeleo ya Sekta ya Nishati katika nchi wanachama.

Taarifa hiyo ya Makatibu Wakuu, iliyowasilishwa kwa Mawaziri hayo imezungumzia  masuala mbalimbali yanayohusu Umeme, Nishati Jadidifu, Mafuta pamoja Gesi.


Baada ya majadiliano hayo, Mawaziri wote wa Sekta ya Nishati wa nchi wanachama wa wameridhia na kusaini makubaliano ya kisekta, kwa lengo la utekelezaji.

Mawaziri walioshiriki mkutano huo ni kutoka nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda pamoja na Burundi.