Yoweri Museveni: 'Afrika ilishindwa kuisaidia Libya ilipovamiwa '


Rais Yoweri Museveni wa Uganda amesema kwamba bara la Afrika lina uwezo wa kuzuia mataifa ya magharibi kuingilia kati ama hata kuvamia mataifa ya Afrika kiholela.

Museveni ambaye alikuwa akizungumza na BBC amesema kwamba ilikuwa makosa kwa mataifa ya magharibi kuivamia Libya na kumng'oa kiongozi wake Muammar Gaddafi bila ya Afrika kuzuia kitendo hicho.

Amesema kwamba viongozi wa Afrika walitumia diplomasia kutatua mzozo huo lakini badala yake wangetumia jeshi lake kukabiliana na wavamizi.

Kiongozi huyo wa Uganda anasema kwamba bara la Afrika lina uwezo mkubwa wa kuweza kuwakabili waliovamia Libya ambayo hadi sada inakumbwa na mzozo wa wenye kwa wenyewe.

''Nawaza Afrika ingeingilia kati na kumpatia mtu funzo, hapo ndipo tulipofeli'', alisema rais huyo anayedaiwa kuwa miongoni mwa viongozi wa Afrika waliokalia madaraka kwa kipindi kirefu kufikia sasa.

Bw. Museveni amesema: ''Lilikuwa shambulio la uvamizi kwani hata mimi mwenyewe sikudhania kwamba mtu anaweza kuwa na mawazo ya kipuzi na kuvamia taifa la Afrika kama walivyofanya''.

''Tatizo ni kwamba tulipatikana wakati mbaya ambapo tulikuwa tumetawanyika hatuakuwa tumejiandaa'', aliongezea.

Amesema kwamba bara la Afrika lina uwezo ambao haujutumika wa kukabiliana na uvamizi wowote kutoka kwa mataifa ya magharibi.

''Iwapo tunataka kuwafurusha wavamizi tunaweza, tuliwafukuza na kuwashinda Wareno na Boers wakati wa ukolini wa mwisho wa karne ya 17 licha ya wao kusaidiwa na mataifa mengi ya kigeni.

Museveni anasema licha ya kukabiliana na wanajeshi wa Muamar Gaddaffi mara mbili nchini Uganda, anasema kwamba kiongozi huyo alikuwa na matatizo yake lakini jinsi alivyotendewa na mataifa ya magharibi ilikuwa makosa makubwa.

Anasema kwamba kulikuwa na njia chungu nzima za kukabiliana na kiongozi huyo na kwamba nguvu zilizotumika dhidi yake zilikuwa mbaya kwa kiongozi wa Afrika aliyekuwa na haiba kama yake.

Kuhusu mazungumzo yanayoendelea kuhusu Libya, Museveni anasema kwamba bara la Afrika lingechukua jukumu la kuangazia maswala yake badala ya kutegemea mataifa ya nje kutafuta suluhu Afrika.

Swala hilo linajiri wakati ambapo Ethiopia na Misri pia zimeamua kuwasilisha tatizo lao la matumizi ya mto Nile Marekani badala ya Muungano wa Afrika.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items