Mji mkuu wa Kinshasa wafungwa wiki tatu DRC sababu ya corona


Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imetangaza kufungwa kabisa kwa mji mkuu wa Kinshasa kwa muda wa wiki tatu ili kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.

DRC imethibitisha kuwa na wagonjwa 54 mjini Kinshasa na kuwaweka watu 2,000 karantini ambao wamehusiana na wagonjwa hao wa covid-19.

Mji huo wa Kinshasa utafungwa rasmi siku ya Jumamosi ambapo hakutakuwa na mtu atakayeruhusiwa kutoka nje siku zaidi ya siku mbili kwa wiki kwa ajili ya kununua mahitaji muhimu ya chakula.

Wakati ambao mji huo utakuwa umefungwa , watumishi wachache wa umma wataruhusiwa kwenda kazini kwa ajili ya majukumu maalumu pamoja na wahudumu wa afya watendelea kwenda kazini.

Aidha wafanyabiashara wameonywa kutopandisha gharama ya vitu wakati huu ambao hali si nzuri.

Wakati huohuo raia wenyewe wameonekana wakilalamikia hatua hiyo ambayo serikali imeichukua kutokana na hali ya maisha ya wengi wanategemea kipato cha dola moja au chini ya hapo.

Wanasema hofu ya hatua hiyo inakuja wakati ambao hali ya kiuchumi katika taifa hilo ni duni.

Hata hivyo jimbo la Kivu ambalo liko mashariki mwa Congo nalo limetangazwa kuwa na mgonjwa mmoja wa corona na kufanya idadi ya maambukizi katika taifa hilo kufika 55.

Mapema wiki hii, rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo alitangaza hali ya dharura na kuufunga mji mkuu wa Kinshasa au kujitenga katika hatua ya kupambana dhidi ya maambukizi ya corona.

Rais Félix Tshisekedi alitangaza kuchukua hatua hizo siku ya Jumanne jioni kupitia televisheni ya taifa.

Bwana Tshisekedi amesema kuwa pamoja na kufunga mipaka ya nchi, kusitisha safari za ndani na nje ya mji mkuu zikiwemo za mabasi, ndege na maji, utekelezaji wa haraka unahitajika.

Wiki iliyopita Jamhuri ya Afrika ya kati ilitoa amri kwa raia wake kutokuwa na mizunguko.

Mpaka sasa DRC imeripotiwa kuwa na wagonjwa 48 wa covid-19 na watu watatu kufariki kutokana na maambukizi ya ugonjwa huo.

Mji mkubwa wa pili wa taifa hilo, Lubumbashi, ulifungwa kwa saa 48-siku ya Jumatatu baada ya watu wawili kukutwa na maambukizi ya Covid-19.

Mmoja alikuwa mwanamume mwenye miaka 47 na mtoto wake wa kiume wa miaka 13, walikuwa wametokea mji mkuu wa Kinshasa siku ya Jumapili.

Na siku hiyohiyo , kifo cha pili kilichotokana na ugonjwa wa corona kilitangazwa na Waziri wa Afya, Eteni Longondo huku wengine 30 walikutwa na maambukizi ya ugonjwa huo tangu Machi 10, 2020.

Gavana wa Lubumbashi alitangaza saa 48 kwa mji wa Lubumbashi kufungwa , kuanzia Jumatatu wakati wakijaribu kubaini abiria 75 ambao walipaswa kutengwa.

Na kutokana na maambukizi hayo wabunge walimshauri Rais Tshisekedi kufunga miji ambayo ina maambukizi zaidi ya virusi vya Corona ambayo ni Kinshasa na Lubumbashi.

Kutokana na maambukizi hayo ya ugonjwa mpya wa Corona, DRC kwa sasa nchi hiyo wameweka marufuku zifuatazo:
Teski kutobeba abiria zaidi ya watatu ingawa hapo awali walikuwa wanaruhusu watu zaidi
Mabasi ya umma ambayo yalikuwa yanabeba watu zaidi ya 60 na sasa wanaruhusiwa kubeba abiria 20 tu