Mkandarasi wa Ghala Akimbia Makatibu Wakuu

MKANDARASI M/s AMI & VAI Investment anayejenga ghala la kuhifadhia mpunga kijiji cha Kigugu wilaya ya Mvomelo amekimbia eneo la mradi baada ya kupata taarifa ya makatibu wakuu wanne kufi ka eneo hilo kukagua mradi huo wa Sh milioni 816.37.

Mradi huo ni sehemu ya mradi mkubwa wa kuongeza thamani zao la mpunga (ERPP) unaoshirikisha wizara mbalimbali zikiwemo Wizara ya Kilimo; Viwanda na Biashara; Ofisi ya Makamu wa Rais( Mazingira) na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

Makatibu hao wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya walipouliza alipo mkandarasi wakati taarifa zimetolewa kwake, walijibiwa kwamba hawaelewi amekwenda wapi kwani alikuwapo hapo.

Msimamizi wa mafundi, Abdul Kabanika akijibu swali la Katibu Mkuu Kusaya uwepo wa mkandarasi alisema, “bosi tulikuwa naye hapa muda mfupi uliopita lakini sasa hatumuoni.”

Katika ziara hiyo iliyoshirikisha pia Katibu Mkuu Profesa Riziki Shemdoe (Viwanda na Biashara), Naibu Katibu Mkuu Balozi Joseph Sokoine (Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira) na Naibu Katibu Mkuu Gerald Mweli (Ofisi ya Rais-Tamisemi) kwa pamoja walimuonya mkanadarasi huyo na kusema watamsaka ili ajieleze kwa nini hajakamilisha mradi huo kwa muda wa mkataba.

Taarifa zinasema kampuni hiyo ya M/s Ami &Vai Investment imeshindwa kumaliza kazi ndani ya mkataba ulioisha Aprili 21, 2020 na ujenzi upo asilimia 70 . Kamati ilikagua pia mradi wa ghala kijiji cha Mbogo Komtongo ambao ujenzi wake umefikia asilimia 70 chini ya mkandarasi M/s Shekemu kwa gharama ya Sh milioni 790.87 lakini nao haujakamilika.

Katibu Mkuu Kusaya alionya na kusema kutokamilika kwa miradi hiyo ni kikwazo kwa wakulima ambao wanahitaji mahali pa kuhifadhi mazao yao na pia lengo la serikali kutotimia. Kutokana na hali hiyo amewaonya wakandarasi waliozembea kukamilisha miradi ya ujenzi wa miundombinu ya skimu za umwagiliaji nchini na hasa wilaya za Mvomero na Kilosa na kusema watachukuliwa hatua za kisheria kwa mujibu wa mikataba waliosaini.

“Hatujaridhishwa kabisa na wakandarasi wa ujenzi wa maghala ya kuhifadhia nafaka ya kijiji cha Mbogo Komtonga na Kigugu hawajakamilisha kazi ndani ya mkataba, ” alisema Kusaya kwa niaba ya kamati hiyo.

Awali kamati hiyo ilitembelea skimu ya umwagiliaji kijiji cha Mvumi wilaya ya Kilosa na kujionea hali ya miundombinu kwa ajili ya mashamba ya mpunga ya wakulima iliyofikia asilimia 84 ya ujenzi mitaro na banio. Skimu hiyo inajengwa kwa gharama ya Sh Bilioni 1.97 na mkandarasi M/s Whitecity International Ltd akishirikiana na M/s Skyline Properties Ltd na kwa mujibu wa mratibu wa mradi kiasi cha Sh milioni 713.15 zimelipwa sawa na asilimia 54.

Alipoulizwa kwa nini mradi haujakamilika msimamizi wa mradi huo, Emanuel Norbet alisema wamechelewa kukamilisha kutokana na uwepo wa mvua nyingi msimu huu zilizoharibu miundombinu ya barabara na mitaro.

Katika hatua nyingine, kamati iliridhishwa na kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa ghala la kuhifadhia mazao kijiji cha Mvumi wilaya ya Kilosa kwa asilimia 99 lililojengwa na mkandarasi M/s B.H Ladwa Ltd kwa gharama ya Sh milioni 971.31 ambapo tayari Sh milioni 536.06 zimelipwa.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Prof. Riziki Shemdoe amewaagiza washauri wasimamizi wa miradi hiyo ambayo haijakamilika kuchukua sheria na kuanza kukata fedha kwa wakandarasi wazembe. “Hatua za kisheria kukata fedha kwa mujibu wa mkataba zichukuliwe haraka,kwani mikataba imeisha na muda wa nyongeza umeisha.

Fedha ya serikali ianze kukatwa kila siku (liqudated damages),” alisema Profesa Shemdoe. Akizungumza hatua alizochukua msimamizi wa miradi ya ujenzi wa maghala Kigugu na Mbogo Komtonga Architect Ismail Mvungi aliwajuisha wajumbe kuwa tayari wameanza kuwakata wakandarasi hao kiasi cha Sh 400,00 kila siku kwa kuchelewa kukamilisha kazi.

Mhandishi wa mradi wa ERPP January Kayumbe alisema miradi hiyo ya ujenzi ilitekelezwa kwa mwaka mmoja na muda wake unamalizika Aprili 21 mwaka huu ,hivyo wakandarasi ambao hawajakamilisha taratibu za sheria zitafuatwa.

Akishukuru kwa niaba ya wananchi Mwenyekiti wa Kijiji cha Kigugu kata ya Sungija wilaya ya Mvomelo, Damas Mnyani alisema miradi hii itasaidia kuongeza uhakika wa upatikanaji maji kwenye mashamba ya mpunga hali itakayoongeza uhakika wa uzalishaji. Mradi huo umefanikiwa hadi sasa kuongeza uzalishaji wa zao la mpunga kutoka tani 2.5 kwa ekari hadi tani 5.5 kwa ekari baada ya miundombinu kuboreshwa.

Mradi wa ERPP ulianza kutekelezwa mwaka mwaka 2015 kwa gharama ya Dola za kimarekani milioni 22.91 toka Benki ya Dunia ukijusisha Tanzania Bara na Zanzibar, ina jumla ya miradi 11 ikiwemo ujenzi wa skimu tano za umwagiliaji, ujenzi wa maghala matano na ujenzi wa maabara moja ya mbegu chini ya ERPP.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items

Kilimo cha Bamia