Tawa Yaongeza Nguvu Kusaka Walioua Nyara Za Serikali

MAMLAKA ya Wanyamapori Tanzania (Tawa) kwa kushirikiana na Uongozi wa Wilaya ya Babati, Polisi na Jumuiya za Hifadhi ya Wanyamapori (WMA) imeongeza nguvu ya kikosi cha ulinzi kuwasaka wahusika wa mauaji ya pundamilia 11 na twiga mmoja yaliyotokea wilayani humo wiki hii.

Mpaka jana hakuna watu waliokamatwa kuhusika na tukio hilo lakini wanadaiwa ni jamii ya wakulima na zaidi ya askari 18 wa Tawa na wengine wa WMA na Polisi wapo eneo la tukio kuhakikisha wahusika wanapatikana. Kwa mujibu wa Tawa, gharama ya twiga ni Dola za Marekani 15,000 (zaidi ya Sh milioni 35) na pundamilia ni Dola za Marekani 1,200 (Sh milioni 2.7).

Mkuu wa Kikosi dhidi ya Ujangili cha Tawa, Kanda ya Kaskazini, Peter Mbanjoko, aliliambia gazeti hili jana kwa simu kuwa, uchunguzi wa tukio hilo unaendelea na wameongeza nguvu ya askari katika eneo la tukio kuwezesha wahusika kutiwa nguvuni. Mbanjoko alisema askari zaidi ya 18 wapo eneo hilo wakishirikiana na askari Polisi, Uongozi wa Wilaya na WMA.

Alisema walipata taarifa ya tukio hilo Aprili 22 mwaka huu na walipofika eneo la Minjingu kwenye mapito ya Wanyamapori (ushoroba) walikuta mizoga ya pundamilia 11 na eneo la Mdolii walikuta twiga ameuawa. Juzi akizungumza na gazeti hili kuhusu tukio hilo, Mbanjoko alisema kosa kama hilo kwa mujibu wa sheria ni la uhujumu uchumi kwa sababu wanyamapori ni rasilimali za Serikali.

Alisema uchunguzi wa awali unaonesha kuwa, waliotenda ujangili huo ni watu jamii ya wakulima, ambao mara nyingi wanalisha mifugo na kulima karibu na maeneo ya matukio hayo. Mbanjoko alisema tayari wamefungua jalada na kuunda kikosi cha uchunguzi kinachowajumuisha Tawa, Polisi, WMA na Wilaya ili kuwasaka wahusika.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items

Kilimo cha Bamia