Asilimia 95 ya Halmashauri zapata hati safi ya usimamizi wa fedha

Mbunge wa Nanyamba, Abdallah Chikota (CCM) aipongeza Serikali kupitia Taarifa ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali(CAG) inaonyesha kuwa kati ya halmashauri 185 ziliokaguliwa halmashauri 176 zimepata hati inayoridhisha sawa na asilimia 95 hatua inayoonyesha nidhamu ya matumizi ya fedha katika mamlaka za serikali za mitaa kuboreka kutokana na usimamizi mzuri katika mamlaka hizo.

Pongezi hizo amezitoa bungeni jijini Dodoma wakati akichangia taarifa ya kamati ya kudumu ya bunge ya hesabu za serikali za mitaa (LAAC) kuhusu taarifa ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za mamalaka za serikali za mitaa kwa mwaka ulioishia juni 30,2019 amesema hayo ni maboresho makubwa na ni tofauti na kipindi cha nyuma.

“Huko nyuma tulipotoka halmashauri nyingi zilikuwa zinapata hati yenye mashaka lakini kwa sasa ni halmashauri 9 sawa na asilimia 5 tu ndio zimepata hati zenye mashaka,hapa unaona kuna nidhamu ya fedha imejengeka katika watendaji wa mamlaka za serikali za mitaa,”ameeleza Chikota.

Aidha Chikota ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa kamati ya LAAC amesema pamoja na maboresho hayo bado kuna maeneo ya kufanyia kazi hasa kwenye taratibu za manunuzi ambapo imeonyesha kuna ukiukwaji wa taratibu za manunuzi.

“Kwenye vitengo vya manunuzi ya serikali za mitaa kumeimarika kwa kiasi kikubwa lakini bado kuna dosari kama CAG alivyoonyesha katika tarfa kuwa amefanya ukaguzi wa kina katika halmashauri 74 na kukuta kuna manunuzi ya Sh bilioni 32.4 yamefanywa bila ya kushindanisha kama sheria ya manunuzi inavyotaka” amesema Chikota.

Chikota ameongeza kuwa CAG pia amefanya ufuatiliaji wa kina kwenye mamlaka za serikali 47 na kukuta manunuzi yamefanyika bila ya kutumia tender board,na hii imechukua kama Sh bilioni  9.2,hapa afisa masuhuli angeweza kuzuia hoja hizi kwa kutumia tender board ambayo ipo kisheria kwenye mamlaka za serikali za mitaa.

Chikota ametoa wito kwa  Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) kufuatilia udhaifu kama huo kwa halmashauri husika ambapo taarifa ya CAG ipo wazi na imezitaja halmashauri hizo.

 Chikota amewataka watendaji wa TAMISEMI kujitathimini kwa nini maafisa masuhuli wameamua kufanya hivi maana wanamrudisha nyuma wazir mwenye dhamana, hoja kama hizi hazikuwa na sababu ya kuwepo kwenye taarifa kama ya CAG.