Matiko: Ningekuwa Waziri Tusingehangaika na Madawati



MBUNGE wa Tarime Mjini kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Esther Matiko,  amesema angekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, nchi ya Tanzania isingepata shida kuhusu suala la madawati kwa wanafunzi kwani wizara hiyo pamoja na wizara ya madini hazijatumia vizuri rasilimali tulizonazo kuliletea maendeleo taifa.

Amesema hayo leo Ijumaa, Mei 22, 2020,  wakati akifanya mahojiano na “Kikao cha Kamati” katika Kipindi cha Front Page kinachoruka kupitia +255 Global Radio.

“Bado hatujafanya vizuri kwenye Sekta ya Utalii, ningekuwa Waziri wa Utalii ningetumia mabalozi wetu walioko nje kuutangaza utajili wetu. Kila Mtanzania angekuwa anaimba utalii wetu kila kona kwa kusifia Mlima Kilimanjaro, Mbuga ya Serengeti, Mikumi na nyingine tulizonazo.

“Kwa rasilimali tulizonazo, Tanzania isingekuwa ikihangaika na suala la uhaba wa madarasa, tuna migodi yenye madini ya aina nyingi karibu kila mkoa, mbuga kubwa za wanyama, makumbusho na vivutio vingi lakini hatujavitumia ipasavyo kutuletea maendeleo.


Kuhusu kutolewa bungeni na kukamatwa

“Kwa miaka yangu mitano Bungeni sijawahi kusimamishwa kuhudhuria vikao vya Bunge, ni siku moja tu Spika Job Ndugai alinitoa tena dakika za mwisho wakati nikipinga deni la Mheshimiwa Godbless Lema, kwa hiyo ninawawakilisha vizuri wananchi wangu wa Tarime Mjini.

Maendeleo aliyoyafanya Tarime

“Tumejenga shule mpya za msingi kumi, za sekondari tatu katika kata nane, tumejenga miundombinu ya barabara za lami zaidi ya km 3 katika mitaa yangu pale Tarime Mjini, mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria, Zahanati ya Kombole, kwa hiyo utaona kabisa Tarime ya 2015 siyo sawa na Tarime ya leo, kwa hiyo wananchi wangu wanajua ninatosha.

Kuhusu kuswekwa mahabusu

“Nilipotoka mahabusu nilieleza bungeni hali ya magereza, nashukuru watu waliokuwa wamewekwa mahabusu kwa muda mrefu, pia watu wenye matatizo ya akili gerezani, waliachiwa. Niliposema ndipo Mheshimiwa Rais akaanza kuzunguka magerezani na kuwaachia, hii inanifariji sana.