Tamwa yatoa salamu za Sikukuu kwa waislamu nchini

Chama cha Waandishiwa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA, ZNZ) kinawatakia waislam wote sikukuu njema ya Mfunguo Mosi baada ya kufunga mwezi mtukufu wa Ramadhani.



Tunaelewa siku hiyo ni siku ya furaha kwa waislam wote nchini husherehekea kwa mipango mbali mbali ikiwemo kuwavisha nguo nzuri watoto wao kwenda kusalimia ndugu na jamaa.



Tunapenda pia kuchukuwa nafasi hii kuwatahadharisha wazazi kuwa karibu sana na watoto wao wakati wa sikukuu ili kujikinga na vitendo vya udhalilishaji.

Katika miaka iliyopita kipindi cha sikukuu huripotiwa kesi nyingi za udhalilishaji kwa wastani wa kesi tano kwa siku ambapo watoto waliopo chini ya umri wa miaka 18 hutoroshwa ama kubakwa.



Pamoja na kuwepo kwa janga la (COVID 19) ambapo kwa mwaka huu sikukuu haitakuwepo rasmi lakini tunaishauri jamii kuwadhibiti watoto ili kuepukana na vitendo hivi viovu ambapo wahalifu hupata fursa kutumia kipindi hichi cha kumalizika kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani kufanya vitendo vyao viovu.



Baadhi ya watoto huonekana wakizurura kwa wingi maarufu kwenda kupokea mkono wa Iddi na hivyo kuhatarisha ustawi wao ambapo wakati mwengine hugonga hata kwenye nyumba wasizokuwa na mahusiano nazo.



Mara nyengine huingia katika nyumba ambazo wanaishi wabakaji na hivyo kuwafanyia vitendo vibaya na pia hata mtaani hurubuniwa kwa kuambiwa wakapewe sikukuu yao.



Hivyo, ni vyema watoto kubakia chini ya uangalizi wa wazee wao kwa wakati wote; mchana na jioni  ili kujilinda kutokana na wabakaji lakini pia dhidi ya maradhi ya corona.



Tunapenda pia kuwakumbusha wananchi kujilinda na maradhi ya corona kwa vile yanaweza kuepukika pindi tukifata maagizo ya wataalamu.