Na Amiri kilagalila,Njombe.
Kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wakulima inayopelekea kukuwa kwa sekta ya kilimo na kusaidia kuongezeka kwa pato la mkulima na Taifa,Kituo cha utafiti wa kilimo (TARI) Uyole,wanasema lengo la kituo kwa sasa ni kuona mkulima Mahiri na anayefanikiwa katika maisha kutokana na kilimo bora na chenye tija.
“Lengo la sasa tunataka mkulima aondoke pale alipo kimaisha,awe mahiri na mkulima huyo tutampima kwa sifa zifuatazo,ambaye atalima kilimo chenye faida,atajitosheleza kwa chakula,ni mkulima ambaye atazalisha mazao kwa ajili ya malighafi ya viwandani,awe ambaye anakuwa na chakula chenye lishe na ambaye hata teteleka na mabadiliko ya hali ya hewa” Dkt.Tulole Lugendo Bucheyeki mkurugenzi wa kituo cha TARI Uyole
Amesema kwa sasa kituo cha Uyole kina aina zaidi ya 8 ya Mahindi zitakazomuwezesha mkulima wa sehemu mbali mbali nchini kufaidika yatakapotunzwa,huku akibainisha kuwa awali walikuwa na mbegu na mbegu kwa ajili Nyanda za juu kusini tofauti na sasa.
“Tuna aina zaidi ya nane ya mbegu za Mahindi ambazo zinaweza zikapandwa sehemu mbali mbali,mwanzoni yalikuwa yanapandwa Nyanda za juu kusini kwa hiyo sasa hivi yanaweza yakpandwa sehemu mbali mbali” Alisema tena Dkt.Tulole Lugendo Bucheyeki mkurugenzi wa kituo cha TARI Uyole
Vile vile amesema kituo kina aina zaidi ya 22 za Maharage huku Soya wakiwa na aina nne.
Lornad Sabula ni mtafiti kutoka taasisi ya utafiti wa kilimo Tanzania kituo cha Uyole na meneja wa mradi wa Pata Tija,anasema kwa sasa wanahitaji kubadilisha mtazamo wa kilimo kwa wakulima zaidi ya laki moja katika mazao ya Mahindi,Maharage na Soya.
“Tunataka mkulima wa Soya ajivunie kuwa mkulima lakini pia mkulima wa Maharage ajivunie kuwa mkulima wa Maharage sambamba na mkulima wa mahindi,kwa maana ya sera ya nchi sasa hivi tunaelekea kwenye uchumi wa viwanda,na viwanda vyetu vitatokana na malighafi yanayotokana na kilimo”alisema Lornad Sabula.
Jafari Mbogela na Anna Wikichi ni wakulima wa kijiji cha Ilunda wanasema wamepata mafanikio makubwa katika kilimo kutokana na matumizi ya Mbegu bora za kilimo kutoka kituo cha utafiti TARI,hali ambayo imewawezesha kupata zaidi ya gunia 50 za mahindi kwa ekari moja tofauti na awali.
“Kuna mabadiliko makubwa kwenye kilimo kwasababu zamani tulikuwa tunatumia mbegu moja tu ile ya kienyeji sasa walipokuja kutufunza wenzetu hawa wa Uyole ukweli mafanikio yapo maana yake na wenyewe wanakuwa humo humo wanatusaidia cha kufanya”alisema Jafari Mbogela
Mpaka sasa mradi wa kuboresha kilimo na maisha ya wakulima umefanikiwa kuwafika wakulima elfu hamsini wa moja kwa moja katika mikoa ya nyanda za juu kusini,huku wengine wakifikiwa kupitia kwa wagani,maonyesho ya kilimo pamoja vyombo vya habari.



