Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF limeonya leo kuwa kupungua kwa fedha za kufadhili msaada wa kiutu nchini Yemen kutasababisha mamilioni ya watoto nchini humo kukumbwa na baa la njaa wakati taifa hilo linakabiliana na janga la virusi vya corona.
Katika taarifa iliyotolewa leo, UNICEF imesema idadi jumla ya watoto wenye utapiamlo walio na umri chini ya miaka mitano kwenye taifa hilo lililoharibiwa kwa vita itaongezeka na kufikia milioni 2.4 mwishoni mwaka mwaka huu, ambayo ni ongezeko la karibu asilimia 20.
Shirika hilo pia limetahadharisha upungufu wa fedha unaweza kusababisha vifo vya watoto wengine 6,600 walio chini ya umri wa miaka 5 ifikapo mwishoni mwa mwaka huu kwa sababu zinazoweza kuzuilika ikiwemo utapiamlo.
UNICEF imesema iwapo dola milioni 54.5 hazitopanikana haraka kusaidia huduma za lishe na afya nchini Yemen, zaidi ya watoto 23,000 wenye utapiamlo sugu watakuwa kwenye hatari kubwa ya kufariki dunia.
