Shirika la Chakula na Kilimo Duniani, FAO, limesema kiwango cha bei ya chakula ulimwenguni kilipanda mwezi Juni ikiwa ni ongezeko la kwanza tangu kuanza kwa mwaka 2020 na kuashiria kuongezeka tena baada ya kushuka kwa kasi kulikosababishwa na janga la virusi vya corona.
Faharasa ya bei ya chakula ya shirika hilo ambayo hupima mabadiliko ya kila mwezi, iliangazia nafaka, mafuta, bidhaa zitokanazo na maziwa, nyama na sukari kwa wastani wa pointi 93.2 mwezi uliopita, hadi asilimia 2.4 mwezi Mei.
Huku kukiwa hakuna uhakika katika soko, bei ya mafuta, sukari na bidhaa zitokanazo na maziwa zimeongezeka tena kwa kiwango cha juu, huku nyama na nafaka zikiwa zimebakia katika bei ya chini.
FAO pia ilirekebisha utabiri wake wa bei ya nafaka kwa mwaka 2020 kwa tani milioni 9.3 ikilinganishwa na tani bilioni 2.790, ambayo ni ongezeko la asilimia 3.0 kwa rekodi ya mavuno ya mwaka 2019.
