https://monetag.com/?ref_id=TTIb Maas: Ujerumani yapinga Urusi kurudishwa G7 | Muungwana BLOG

Maas: Ujerumani yapinga Urusi kurudishwa G7


Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas anasema haoni uwezekano wa Urusi kurudi katika muungano wa nchi saba zilizoendelea kiviwanda duniani G7 hivi karibuni.

Hii ni baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kuzungumzia wazo la kuiruhusu Moscow kujiunga tena na muungano huo.

Katika taarifa iliyochapishwa leo na magazeti mawili ya Ujerumani Rheinische Post na Bonner General-Anzeiger, Maas amesema Urusi haiwezi kukubaliwa kurudi kwenye muungano huo kwani sababu zilizopelekea Urusi kuondolewa ni uvamizi wake wa eneo la Crimea na mapigano inayoyafanya mashariki mwa Ukraine na endapo hakutakuwa na suluhu basi hakuna uwezekano wa Urusi kujiunga tena na G7.

Trump amependekeza kutanuliwa kwa muungano wa G7 na amesema anataka kuzialika Australia, India, Urusi na Korea Kusini katika mkutano ujao.

Rais huyo wa Marekani anapanga kuufanya mkutano huo mwezi Septemba baada ya kuahirishwa kutokana na virusi vya corona.