Mwaka 2001 Marekani iliishambulia kijeshi na kuikalia kwa mabavu Afghanistan kwa kutumia kisingizio cha mashambulio ya Septemba 11 yaliyolenga sehemu kadhaa ndani ya ardhi ya Marekani. Wakati rais wa Marekani Donald Trump alipokuwa katika kampeni za uchaguzi wa urais wa mwaka 2016 na hata baada ya kuingia ikulu ya White House aliahidi kuwa atawaondoa askari wa nchi hiyo walioko Afghanistan. Hata hivyo pamoja na ahadi hiyo, askari wengi wa jeshi la Marekani wangaliko katika ardhi ya Afghanistan.
Hivi sasa maafisa waandamizi wa serikali ya Marekani wakiwemo wa wizara ya ulinzi ya nchi hiyo Pentagon wanaielekezea kidole cha tuhuma Russia kuwa inaingilia masuala ya Afghanistan na inashirikiana pia na Taliban ili kwa njia hiyo wapate kisingizio cha kutetea kushindwa kwa Washington na kupata sababu ya kuendelea kuwepo kijeshi nchini humo. Miongoni mwa viongozi wa Marekani walioituhumu Russia ni waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Mike Pompeo ambaye amesema, Russia inapinga Marekani kuwepo Afghanistan na inaliuzia silaha kundi la Taliban. Akiongea na waandishi wa habari Pompeo amesema: "Ni ukweli kwamba Russia inafanya mambo yake Afghanistan ili kukabiliana na Marekani; na hili si jambo jipya. Kwa miaka 10 Warussia wanaiuzia Taliban silaha mbalimbali na jambo hili linahatarisha maisha ya Wamarekani. Tumelalamikia suala hili na kila nilipokutana na mwenzangu wa Russia nimekuwa nikimwambia: "Simamisheni jambo hili."
Hata hivyo Russia imekanusha mara kadhaa madai ya Marekani kwamba inawauzia silaha Taliban.
Katika msimamo mwengine ulioonyeshwa na Marekani, siku ya Jumatano wizara ya ulinzi ya nchi hiyo Pentagon ilitoa ripoti ikidai kwamba, serikali ya Russia imeshirikiana na Taliban kwa ajili ya "kuharakisha kuondoka askari wa Marekani" nchini Afghanistan. Katika ripoti hiyo iliyopewa jina la "Uimarishaji usalama na uthabiti Afghanistan", Pentagon imedai kuwa, Moscow inashirikiana na Taliban kuidhoofisha serikali ya Afghanistan. Katika ripoti hiyo ya Pentagon imedaiwa kuwa: "Russia inaisaidia kisiasa Taliban ili kuwa na ushawishi ndani ya kundi hilo, kufupisha muda wa kuwepo kijeshi askari wa Magharibi na kuimarisha operesheni dhidi ya DAESH (ISIS), ijapokuwa katika duru rasmi inakanusha kuwepo kwa mahusiano hayo." Baadhi ya wachambuzi wanasema, ripoti hiyo mpya ya Pentagon ina maana ya kutangaza rasmi madai ya kuwepo uhusiano kati ya Russia na Taliban.
Msimamo huo wa madai dhidi ya Russia umechukuliwa huku Kongresi ya Marekani na wabunge wa chama wa Democrat hususan Spika wa Baraza la Wawakilishi Nancy Pelosi akitaka zichukuliwe hatua kali dhidi ya Moscow hasa za kuiwekea vikwazo nchi hiyo. Bi Pelosi amechukua msimamo huo kufuatia ripoti iliyochapishwa hivi karibuni na gazeti la New York Times iliyoeleza kwamba, idara ya intelijensia ya jeshi la Russia ijulikanayo kwa ufupi kama GRU ilifanya muamala na Taliban huko nyuma na kuwaahidi kuwa itawapatia bakhshishi ya fedha taslimu kwa kila askari mmoja wa Marekani watakayemuua huko Afghanistan. Kwa mujibu wa madai yaliyotolewa na gazeti hilo, maafisa wa intelijensia wa Marekani walimjulisha rais wa nchi hiyo Donald Trump kuhusu hatua hiyo ya Russia. Ripoti hiyo ya New York Times ilichapishwa tena baadaye na magazeti ya Washington Post na Wall Street Journal kwa kunukuu "duru za ndani ya White House".

