Tanzania yataja vipaumbele vilivyopelekea kupaa kufika uchumi wa kati



Serikali imesema utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkati iliyowagusa wananchi na kusaidia kupata vipato ni moja ya vitu vilivyosaidia nchi kupaa na kufikia nchi za uchumi wa kati.

Hapo Jana Banki ya Dunia imetangaza Tanzania kuwa miongoni mwa nchi za kipato Cha kati ambapo umepanda kutoka kuwa nchi masikini na kuwa miongoni mwa nchi 50 za uchumi wa kati .

Akizungumza na wanahabari leo July 2, 2020, jijini Dodoma, Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt Hasan Abbas, amesema kitendo cha nchi kutekeleza miradi mikubwa imechangia kukua kwa kipato cha mtu mmoja mmoja na kupelekea kuingia katika nchi za uchumi wa kati.

Ametaja baadhi ya mambo ambayo yamesaidia kwa nchi kupaa ni amani na utulivu katika nchi na kubainisha kuwa viongozi wa nchi wamekuwa wakisimamia amani na utulivu ndivyo vilivyosababisha nchi kupaa.

"sisi Kama nchi tumesimamia amani na utulivu na tumetekeleza miradi mikubwa Kama reli ya kisasa na mingine iliyoajiri watanzania wengi na umeongeza kipato cha mtu mmoja mmoja" amesema Dkt Abbas.

Ametaja vitu vingine vilivyosaidia kwa nchi kupaa ni mipango mathabiti iliyotekelezwa, kufanya maamuzi magumu yaliyoleta tija na kuwasaidia watanzania.

"Watanzania wengi mmeona kuna baadhi ya nchi zilitaka tufuate mwelekeo wao na sisi tukakataa na hasa katika suala la corona tulifanya maamuzi magumu na Sasa matokeo yake mmeyaona, bila uthubuti tusingekuwa hapa tulipo" amesema.

Ametaja sababu nyingine kuwa ni adhima ya nchi ya kujitegemea, misingi katika matumizi ya fedha za serikali na hasa katika kuzuia safari za nje zilizokuwa zikitumia fedha nyingi.

Nyingine ni kuwekeza katika elimu kuhakikisha watanzania wanapata elimu bora na sio bora elimu, pamoja na kuthamini sekta binafsi katika kuleta maendeleo ambapo amesema adhima ya serikali ni kuboresha zaidi sekta binafsi kwa kuondoa tozo zinazowakwaza.

Aidha amewataka watanzania kujitathmini Mara baada ya nchi kuingia katika uchumi wa kati kwa kuwa na mabadiliko katika nyanja za maisha, kifikra na kubadilisha mtindo wao wa maisha.