Wapalestina waandamana Gaza kulaani uporaji wa ardhi zao


Maelfu ya wananchi wa Palestina katika Ukanda wa Gaza jana Jumatano walifanya maandamano makubwa ya kulaani mpango wa utawala wa Kizayuni wa Israel wa kutaka kutwaa ardhi ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Waandamanaji hao wametoa mwito wa kukamatwa na kufikishwa mbele ya sheria maafisa wa utawala huo pandikizi, kutokana na jinai zisizo za kiutu wanazowafanyia wananchi madhulumu wa Palestina.

Viongozi wa makundi ya muqawama walioshiriki maandamano hayo ya jana katika Ukanda wa Gaza wamesema njia pekee ya kuzuia kuporwa ardhi zaidi za Wapalestina ni kuendelea kufungamana na harakati za mapambano na kusimama kidete.

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) jana ilifyatua baharini maroketi kama ishara ya kuuonya utawala haramu wa Israel, dhidi ya kutekeleza mpango wake huo batili ambao umekosolewa katika kila kona ya dunia.


Kutokana na mashinikizo ya jamii ya kimataifa na maonyo yalitolewa na makundi ya muqawama katika eneo la Asia Magharibi, utawala wa Kizayuni wa Israel ambao upo katika njia panda, hapo jana ulishindwa kuanza kutekeleza mpango huo wa kutwaa maeneo ya Ukingo wa Magharibi na kuyaunganisha na ardhi za Palestina zilizoghusubiwa.

Utawala huo ghasibu umedai kuwa umeakhirisha mpango huo ambao Waziri Mkuu, Benjamin Netanyahu alidai kuwa unapaswa kuanza kutekelezwa Julai Mosi, eti kutokana na janga la corona.