Aua mchepuko na mtoto baada ya kuufumania nyumbani kwake na rafiki yake

Na Clavery Christian Bukoba Kagera.
Jeshi la polisi mkoani Kagera linamshikilia kijana mmoja aitwaye Derick Dambuve mwenye umri wa 26 kwa kumuua mkwe wa mtu, Helda Amon (28) na mwanae Gradnes Amon (2) baada Helda kufumaniwa akifanya tendo la ndoa na Kajere Ibrahim (mchepuko mwingine) nyumbani kwa Derick.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Kagera, Revocatus Malimi amesema kuwa tukio hilo limetokea Agosti 22, mwaka huu kijiji cha Mukoma wilaya ya Ngara mkoani Kagera na uchunguzi wa awali umebainisha kuwa Helda alikuwa mke wa mtu, yeye na mwanae Gradnes walikwenda kijiji cha Mukoma kwa ajili ya kushiriki mnada wa gulio, akiwa gulioni hapo aliingia kwenye kilabu cha pombe ambako ndiko alikokutana na Derick na kuanzisha mahusiano.

"Baada ya kuanzisha mahusiano siku hiyo hiyo walikubaliana kuwa wangekuwa pamoja usiku huo, ndipo Derick alipomkabidhi Helda kwa rafiki yake (Alex Gray) ili mpeleke nyumbani kwake atamkuta baada ya kumalizia kufanya kazi ya ujenzi ambayo alikuwa hajaikamilisha.

Derick aliacha amewanunulia pombe akaenda kumalizia kibarua chake, walipomaliza kinywaji Alex alimpeleka Helda nyumbani kwa Derick na kufikisha salama akamuacha akimsubiria mwenyeji wake," alisema Malimi.

Malimi alisema wakati Helda na mwanae wanaendelea kumsubiri Derick nyumbani hapo ndipo Kajere alipofika ambaye naye alimuomba Helda waanzishe mahusiano ombi ambalo lilikubaliwa na kuanza kutenda tendo la ndoa.

"Wakati wakiendelea kutenda tendo la ndoa nyumbani kwa Derick ndipo Derick mwenyewe aliporudi nyumbani na kuwakuta bado hawajamaliza na baada ya Kajere kugundua kuwa wamefumaniwa alifanikiwa kumkimbia na kumuacha Helda.

Kufuatia fumanizi hilo, Derick alimpiga Helda kwa kutumia silaha mbalimbali ikiwemo kifaa cha mazoezi cha kunyanyua kwa ajili ya kutunisha kifua na kumsababishia mauti.

Baada ya Derick kuwa tayari amemuua Helda, naye mtoto Gradnes alianza kulia jambo lililosababishia Derick hasira na kuanza kumshambulia kwa kumpiga na kifaa hicho cha mazoezi na kusababisha kifo cha mtoto huyo."

Malimi alisema kwa sasa Derick anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya Helda na mtoto wake Gradnes na upelelezi ukikamilika atafikishwa mahakani kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za kisheria.