Mbunge Mteule wa Jimbo la Butiama Jumanne Sagini amesema zamani walikua wanatumia masaa 12 kwa basi kutoka Musoma mpaka Mwanza ila kwa sasa ni safari ya masaa matatu tu baada ya waziri wa ujenzi wa kipindi hicho ambaye ndio Rais John Magufuli kutengeneza barabara kiwango cha lami.
Akizungumza kwenye mkutano wake wa kampeni uliofanyika Kijiji cha Kibubwa Kata ya Butuguri amesema kuwa Rais anatambua miundombinu ya barabara kuwa ndio moja wapo ya misingi ya kufungua uchumi wa nchi.
"Bila Rais Magufuli kajenga barabara za kutosha mijini na vijijini hali ya kiuchumi kwa wafanyabiashara ingekuwa mbaya sana na nyie wakulima na wafugaji pia ni mashaidi kwa sababu mnatumia barabara kupitisha mifugo na kusafirisha mazao yenu kwenda sokoni kwa bila kukwama njiani," amesema Sagini.
Sagini ameeleza kuwa anashangaa kuona baadhi ya wanasiasa wakipinga miundombinu hiyo wakati wanaitumia kila siku na inawasaidia kufanya mambo yao kwa wakati.
Aidha amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura za kutosha mgombea urais kupitia CCM ifikapo tarehe 28 Oktoba, mwaka huu ili akamilishe miundombinu ya barabara ambayo haikukamilika.