Wakala wa viwango vya madeni, Moody's, umeshusha kiwango cha uwezo wa kukopesheka cha Uingereza kwa alama moja, hali inayoashiria madhara ya nchi hiyo kujitowa kwenye Umoja wa Ulaya, na pia athari ya janga la virusi vya corona.
Kwa mujibu wa wakala huo, Uingereza sasa inashikilia nafasi ya Aa3, na sio tena Aa2, licha ya kwamba muonekano wake umeondoka, kutoka hasi na kuwa tulivu.
Taarifa iliyotolewa jana jioni na wakala huo, imesadifiana na tamko la Waziri Mkuu Borris Johnson, linaloashiria kwamba huenda Uingereza na Umoja wa Ulaya, zikashindwa kupata makubaliano ya kibiashara.
Uingereza ilijiondowa rasmi kutoka Umoja wa Ulaya, tarehe 31 Januari mwaka huu, kufuatia kura ya maoni ya mwaka 2016.
Janga la COVID-19, nalo limeongeza madeni ya nchi hiyo, na linahofiwa kuwa litaendelea kuathiri moja kwa moja, uwezo wake wa uzalishaji kwa kipindi kirefu kijacho.
