Majitaka kupewa kipaumbele sekta ya maji

Naibu Katibu Mkuu, Mhandisi Nadhifa Kemikimba ameitaka Jumuiya ya Wasambazaji Maji Tanzania (ATAWAS) kutoa kipaumbele kwenye eneo la majitaka baada ya kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kwenye eneo la usambazaji wa majisafi.

Mhandisi Kemikimba ametoa maelekezo hayo katika uzinduzi wa Kongamano la 8 la Maji katika ukumbi wa mikutano wa St. Gasper, jijini Dodoma.

“Kuna mafanikio makubwa kwa upande wa usambazaji maji, lakini kwa upande wa majitaka bado. ATAWAS mnatakiwa kuwekeza kiasi kikubwa kwenye eneo hili, ambapo lengo letu ni kufikia asilimia 30 ifikapo mwaka 2025 kwa sababu majisafi ni mengi na itachangia kuwepo kwa majitaka mengi “, amezungumza Naibu Katibu Mkuu.


“Serikali ipo tayari kutoa ushirikiano ili kufanikisha azma hiyo, lakini pia ni lazima katika majadiliano yenu muweke msisitizo kwenye utafiti na ubunifu kwa kuwatumia Taasisi za Elimu ya Juu ili kuweza kupata suluhisho la kudumu litakalomaliza changamoto zote”, amesisitiza Mhandisi Kemikimba.

Kadhalika, Naibu Katibu Mkuu ametoa wito kwa wadau wote wa Sekta ya Maji nchini kushirikiana na ATAWAS ili kufanikisha utekelezaji wa miradi ya maji kwa sababu peke yao hawatafanikiwa.


Aidha, Mwenyekiti wa Bodi ya ATAWAS na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tanga (Tanga UWASA), Mhandisi Geofrey Hilly amesema ATAWAS imezindua rasmi mpango wa kuwajengea uwezo wanachama wake kwenye eneo la menejimenti ya rasilimali fedha, ukizingatia kuwa miongoni mwa changamoto kubwa ambazo zinazozikabili Mamlaka za Maji na sekta kwa ujumla, ni usimamizi wa fedha za utekelezaji wa miradi mijini na vijijini.

Pia, ameongeza kuwa ATAWAS pamoja na Taasisi za Elimu ya Juu zimeshasaini mkataba wa ushirikiano kwenye eneo la utafiti kwa lengo la kupata suluhisho la kudumu changamoto za kisekta.


Lengo la Kongamano hilo ni kujadiliana, kutathimini na kuzipatia ufumbuzi  changamoto za kisekta na kubaini fursa zilizopo ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kufikia  dira ya Taifa ya mwaka 2025, pamoja na lengo la sita (6) la Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa kwa mwaka 2030.

 

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items

Ujuwe Ugonjwa wa Busha

Kilimo cha Bamia