Rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo anakwenda Ethiopia leo kuongoza juhudi za upatanishi kwenye mzozo kati ya serikali kuu na jimbo la kaskazini la Tigray.
Msemaji wake ameliambia shirika la habari la AFP kuwa Obasanjo tayari yuko njiani kwenda mjini Addis Ababa kwa utatuzi wa mzozo unaoendelea lakini hakutoa maelezo zaidi.
Hata hivyo serikali ya Ethiopia na Umoja wa Afrika zimesema kwa pamoja kuwa hazina taarifa juu ya ziara hiyo ya Obasanjo ambaye hapo kabla aliwahi kuwa mjumbe maalum wa amani wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Katika hatua nyingine ofisi ya waziri mkuu wa Ethiopia ilikanusha mapema leo taarifa za maafisa wa serikali ya Uganda kuwa rais Yoweri Museveni wa nchi hiyo atakutana na wawakilishi wa pande hasimu kuratibu mazungumzo ya amani.
