Ni miezi nane sasa tangu mpaka wa Rusizi-Bukavu kufungwa, maelfu ya watu ambao walikuwa wanalazimika kuvuka kwenda Bukavu nchini DRC kutoka mji wa Rusizi nchini Rwanda, wanasema maisha yamekuwa magumu sana kwao.
Mipaka ilifungwa tangu mwezi Machi, kwa sababu ya janga la corona.
Hivi karibuni ,Rwanda na DRC walikubaliana kufungua mpaka kwa idadi ndogo ya watu walio na sababu maalum huku watu hao wakijigharamia katika vipimo vya Covid 19.
Jambo ambalo halijaleta mabadiliko makubwa katika upande wa ajira ,kwa kuwa idadi ni ndogo bado.
Wananchi wa eneo hilo wanasema hali ya kiuchumi na maisha yamebadilika mno hakuna aliyepata msaada wa chakula serikalini wakati wa sheria ya kutotoka nyumbani. "Maisha yalisimama kwa sababu mpaka huu ndio ulikuwa riziki yetu.’’
"Badala yake, tuna madeni mengi,tumekuwa omba omba ...mara kilo ya sukari ,mara mchele ili kunusuru maisha ya watoto yaani tuko katika maisha magumu’’ Uwamahoro Olive anasema alikuwa akivuka mpaka kila siku kwenda Bukavu kufanya kazi ya kutengeneza bustani.
‘’Mimi kazi yangu ni ya kutengeneza bustani, nilifanya kazi hiyo mjini Bukavu kwa miaka 8 sasa. .ni kazi iliyokuwa inaingiza kila mwezi nilikuwa napata takriban dolla 80.Tangu mipaka kufungwa tunahangaika sana hata kupata chakula ni shida’’,alisema mkazi mwingine.
Fundi mwingine wa ujenzi anayeishi katika mji wa Rusizi alisema: "Kule Congo kuna kazi nyingi za kufanywa, hata wakati mwingine wanakuita wenyewe kwa ajili ya kazi ,huwezi kuenda Congo na kurudi nyumbani mikono mitupu.’’ Rwanda imeishafungua viwanja vya ndege, lakini haijafahamika lini itakapofungua mipaka ya ardhini.
