Lilian Stanley, mtuhumiwa wa kuiba mtoto mchanga mjini hapa amefikishwa mahakamani.
Lilian ambaye ni mkazi wa Uwanja wa Taifa mjini hapa, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro kwa tuhuma ya kuiba mtoto mchanga mwenye umri wa mwezi mmoja.
Anatuhumiwa kumwiba mtoto huyo kutoka kwa mama yake, Neema Seleman (27) katika Kanisa la Ufufuo na Uzima lililopo Kihonda mkoani hapa.
Mashtaka ya Lilian yalisomwa na mwendesha mashtaka wa Serikali, Evelyne Ndunguru mbele ya hakimu mkazi mfawidhi, Maua Hamduni. Mtuhumiwa anadaiwa kuwa Desemba 24 mwaka jana alimwiba mtoto huyo kutoka kwa mama yake wakiwa kanisani.
Evelyne alisema mshtakiwa alitenda kosa hilo kinyume na sheria na kanuni ya adhabu.
Akitaja shtaka hilo, hakimu Hamduni alisema dhamana ipo wazi kwa mtuhumiwa na kwamba kesi hiyo imetajwa kwa mara ya pili baada ya mshtakiwa kufikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Desemba 29.
