Wataalam kutoka Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) watasafiri China Januari 14 ili kuchunguza chanzo cha mlipuko wa janga la virusi vya corona (Covid-19).
Tume ya Kitaifa ya Afya ya China ilitoa taarifa fupi juu ya ziara ya wataalam hao wa WHO watakaosafiri nchini.
Katika taarifa hiyo, iliarifiwa kwamba wataalam wa WHO watakutana na wataalam wenzao wa China wakati wa ziara hiyo.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Hua Chunying alitangaza katika mkutano aliofanya na waandishi wa habari Januari 6 kwamba mashauriano yalifanywa na shirika hilo juu ya suala la kuchunguza chanzo cha Covid-19.
Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dr. Tedros Adhanom Ghebreyesus alitoa maelezo mnamo Januari 5 kuhusu hali ya wataalamu wa kimataifa ambao wanatarajiwa kwenda China kuchunguza asili ya Covid-19 na kusema,
"Tuligundua kwamba maafisa wa China bado hawajakamilisha idhini ya vibali muhimu vya wajumbe watakaokwenda China. Taarifa hii imenikatisha tamaa sana kwa kuwa wajumbe wawili wa timu tayari walikuwa wameanza safari yao (kwenda China) na wengine wakazuiwa kusafiri dakika za mwisho."
Mike Ryan ambaye ni Mkurugenzi wa Mipango ya Dharura ya WHO, alisema kuwa tatizo la visa lilizuia wajumbe wa kisayansi wa WHO kuingia China.
