Urusi imesisitiza leo kuwa haitokubali uingiliaji wa nchi nyingine katika mambo yake ya ndani, ikimaanisha miito ya jamii ya kimataifa ambayo imelaani kufungwa jela kiongozi wa upinzani wa Urusi Alexei Navalny.
Msemaji wa Ikulu ya Rais Dmitry Peskov amewaambia wanahabari kuwa Urusi haitozingatia taarifa zozote zinazohusu matumizi ya sheria za nchi dhidi ya wanaozikiuka, pamoja na hukumu za mahakama za Urusi.
Kauli ya serikali imekuja wakati Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell akielekea leo mjini Moscow katika ziara itakayogubikwa na kufungwa jela kwa Navalny na ukandamizaji unaofanywa dhidi ya waandamanaji wanaomuunga mkono.
Ziara hiyo ambayo ni ya kwanza kufanywa na mjumbe wa ngazi ya juu wa Umoja wa Ulaya nchini Urusi tangu 2017, imezusha shutuma kutoka kwa baadhi ya mataifa ya Ulaya yanayohofia kuwa Urusi itaitumia kama ushahidi kuwa Umoja wa Ulaya unataka kurejesha hali ya kawaida.
