Umoja wa Mataifa umesema hakuna maelewano ya kutosha ya kuanza tena mazungumzo kuhusu Cyprus, baada ya mkutano wa kilele wa siku tatu unaojaribu kuumaliza mkwamo wa miaka minne kupitia mazungumzo ya amani.
Wanadiplomasia wamekuwa wakijaribu kutafuta muafaka wa kumaliza mzozo wa miongo kadhaa kati ya Wacyprus wa Ugiriki na Uturuki ambao unadhoofisha eneo la mashariki mwa Mediterania na ni chanzo kikubwa cha mvutano kati ya washirika wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO Ugiriki na Uturuki.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema mjini Geneva kuwa watafanya juhudi upya labda katika miezi miwili au mitatu.
Cyprus iligawanywa mara mbili katika uvamizi uliofanywa na Uturuki mwaka wa 1974 ukichochewa na mapinduzi mafupi yaliyopangwa na Ugiriki.
Serikali ya kugawana madaraka kati ya Wacyprus wa Ugiriki na Uturuki ilivunjika, miaka mitatu tu baada ya uhuru kutoka kwa Uingereza katika mwaka wa 1960.
