Tofauti miongoni mwa viongozi wa Umoja wa Ulaya kuhusu jinsi ya kuishughulikia Urusi zimeshuhudiwa leo wakati wakianza mazungumzo yao ya siku mbili mjini Brussels, ambayo pia yataangazia mahusiano yao magumu na Uturuki.
Wakati Ufaransa na Ujerumani zikihimiza kukuza mahusiano na Moscow, pendekezo la nchi hizo mbili la kufanyika mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya na Urusi linapingwa na mataifa kadhaa wanachama.
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani anasema Umoja wa Ulaya unapaswa kutafuta mbinu za kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na Rais wa Urusi Vladmir Putin.
Naye Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa alitoa mfano wa mkutano wa Rais Joe Biden wa Marekani na Putin mjini Geneva.
Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell alionya kuwa mahusiano yapo katika mkondo wa kuharibika zaidi.
Lakini nchi nyingine kadhaa kama vile Lithuania zimeonyesha mashaka juu ya kujongeleana na Urusi, na zimehimiza tahadhari.
