China leo imeshusha kiwango cha uhusiano wake wa kidiplomasia na Lithuania na kuelezea kutoridhishwa kwake na taifa hilo kwa kuiruhusu Taiwan kufungua ubalozi mdogo usio rasmi nchini humo na kuibua mvutano katika mzozo ambao umeihusisha Marekani.
Katika taarifa, wizara ya mambo ya nje ya China imesema, Lithuania imepuuza msimamo wa China na kanuni za kimsingi za uhusiano wa kimataifa.
Taarifa hiyo imeongeza kusema kwamba hatua ya Lithuania imehujumu uhuru na uadilifu wa kimipaka wa China na kuingilia kwa kiwango kikubwa masuala ya ndani ya taifa hilo hali inayosababisha mfano mbaya kimataifa.
Wizara hiyo imeihimiza Lithuania kusahihisha makosa yake mara moja na kutodharau azimio la watu wa China la maamuzi ya kulinda uhuru wa taifa hilo na uadilifu wa mipaka yake. China imesema itakuwa na mwakilishi wa ngazi ya chini wa kusimamia masuala ya kidiplomasia nchini humo badala ya balozi.