Waziri mkuu wa Poland Mateusz Morawiecki leo ameutaja mzozo wa wahamiaji katika mpaka kati ya taifa lake na Poland kwenye mpaka wa Mashariki wa Umoja wa Ulaya, kuwa jaribio kubwa zaidi la kuiyumbisha Ulaya tangu enzi za vita baridi miaka 30 iliyopita.
Katika ujumbe kupitia ukurasa wake wa twitter, Morawiecko amesema rais wa Belarus Alexander Lukashenko alianzisha vita vikubwa dhidi ya Umoja wa Ulaya na kwamba Poland haitokubali hujuma na itafanya kila juhudi kulinda mipaka ya Umoja huo.
Wakati huo huo, Morawiecki amesema atafanya mfululizo wa mazungumzo barani Ulaya kuhusu mgogoro wa wahamiaji kwenye mpaka wake na Belarus, ambao anatarajia utaendelea kwa muda mrefu.
Morawiecki amesema atakutana na wanachama wenzake wa Umoja wa Ulaya Lithuania, Latvia na Estonia, ambao pia wamekuwa wakiathiriwa na shinikizo la wahamiaji katika miezi ya hivi karibuni, ingawa kwa kiwango kidogo.