Ikulu ya Kremlin imeyashtumu mataifa ya Magharibi kwa kuchochea mivutano nchini Ukraine kwa kutoa taarifa za mara kwa mara zinazodai kuwa Urusi inajiandaa kuishambulia Ukraine. Urusi imeihimiza Marekani na washirika wake kukomesha kutoa kauli za kuzua hofu na kuchochea mivutano.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken mnamo siku ya Jumamosi alisema Washington ina wasiwasi juu ya shughuli za vikosi vya jeshi la Urusi kwenye mpaka wake na Ukraine, baada ya Ukraine kusema inahofia kuwa Urusi inaweza kufanya shambulio.
Maafisa wa Marekani, wale wa muungano wa kujihami wa NATO pamoja na wa Ukraine pia wamekuwa wakitoa kauli kama hizo kwa takriban wiki mbili sasa, kwa kile walichokitaja ni harakati zisizo za kawaida za wanajeshi wa Urusi karibu na mpaka wa Ukraine. Urusi hata hivyo imekanusha madai hayo na kusema kauli kama hizo ni za uchochezi.