Wafanyakazi TUGHE Tawi la Uhamiani wajadili rasimu ya bajeti ya Uhamiaji mwaka 2024/25


Na. Konstebo Josephat Mtema, Dar es Salaam


Baraza la Wafanyakazi TUGHE Tawi la Uhamiani leo tarehe 29 Aprili 2024 limefanya kikao cha kujadili Rasimu ya Bajeti ya Idara ya Uhamiaji kwa Mwaka wa fedha 2024/2025, kikao hicho kimefanyika katika Ukumbi wa Baraza la Maaskofu (TEC) Kurasini Jijini Dar es salaam na kufunguliwa na Mgeni Rasmi Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Bw. Ally Sengo Gugu.

Akitoa Hotuba yake kwa wajumbe wa Baraza hilo Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Bw. Ally Gugu aliipongeza Idara ya Uhamiaji kwa kuendelea kutekeleza vyema Majukumu yake kwa Utii, Uhodari na Weledi wa hali ya juu sanjari na kushirikiana vyema katika kusimamia miradi ya Maendeleo kwa faida ya Uhamiaji na Taifa kwa ujumla.

"Nasisitiza Mshikamano na Umoja katika Majukumu yetu ya kila siku kwani ndio msingi wa utendaji kazi wetu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na majadiliano mtakayofanya hapa nategemea mtatupatia Wizara kama michango ya kuboresha katika kuelekea kusomwa kwa Bajeti ya Wizara Bungeni Jijini Dodoma Bajeti ambayo imezingatia mambo ya msingi yanayohusu Watumishi na kazi itafanyika ipasavyo" Alisema Bw. Gugu

Aidha aliongeza kwamba Baraza la Wafanyakazi ndani ya Idara ya Uhamiaji ndicho chombo mahususi kinachoweka misingi ya kuhakikisha kwamba HAKI na MASLAHI ya Maafisa, Askari na Watumishi Raia yanazingatiwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za zilizopo.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Kamishna Jenerali wa Uhamiaji na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi Tawi la Uhamiaji Kamishna wa Uhamiaji Divisheni ya Uraia na Pasipoti (CI) Gerald Kihinga alisema, ajenda kuu pamoja na mambo mengine ilikuwa ni kuwasilisha Taarifa ya utekelezaji wa majukumu mbali mbali ya Idara ya Uhamiaji kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2023/2024 na kujadili Rasimu ya Bajeti ya Uhamiaji kwa Mwaka wa fedha 2024/2025.

Baraza hilo limekuwa likileta ufanisi mkubwa katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya Idara ya Uhamiaji hususani katika kuunganisha, kuelimisha, kutetea haki, wajibu na maslahi ya Wanachama kwa wakati.

Post a Comment

0 Comments