Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) ina jukumu la kuendeleza na kusimamia masoko ya mitaji hapa nchini, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba shughuli katika masoko ya mitaji zinafanyika kwa kufuata sheria, taratibu na miongozo ili kuleta uwazi na haki kwa washiriki wote.Bwa. Alfred Mkombo Mkurugenzi wa Utafiti, Sera na Mipango akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa Mfuko wa Uwekezaji wa pamoja wa Timiza (Timiza Fund) wa Kampuni ya ZAN SECURITIES LIMITE leo Mei 27, 2024
Masoko ya mitaji ni sehemu ya mfumo wa sekta ya fedha inayowezesha upatikanaji wa fedha za muda mrefu, yaani zaidi ya mwaka mmoja, kwa ajili ya kugharamia shughuli za maendeleo. Fedha za kugharamia shughuli za maendeleo hupatikana kwa kuuza hisa za kampuni (shares), hatifungani za kampuni (corporate bonds), hatifungani za taasisi (Subnational Bonds), hatifungani za Serikali (Government bonds) na vipande katika Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja (Collective Investment Schemes). Fedha hupatikana kutoka kwa wawekezaji, ambao ni watu binafsi, taasisi na kampuni na hatimaye fedha hizo huwekezwa katika sekta za uzalishaji na hivyo kuchochea ustawi na maendeleo ya uchumi.
Aidha utekelezaji wa mipango na mikakati ya Serikali imekuwa na matokeo chanya katika maendeleo ya Sekta ya Fedha, hususan masoko ya mitaji ambapo thamani ya uwekezaji katika masoko ya mitaji imeongezeka kwa asilimia 23.2 na kufikia shilingi trilioni 43.4 katika kipindi kilichoishia Aprili 2024, ikilinganishwa na shilingi trilioni 35.2 katika kipindi kilichoishia Aprili 2023.
Jumla ya mauzo ya hisa na hatifungani yameongezeka kwa asilimia 64.5 na kufikia shilingi trilioni 4.2 katika kipindi kilichoishia Aprili 2024, ikilinganishwa na shilingi trilioni 2.5 katika kipindi kilichoishia Aprili 2023. Thamani ya Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja imeongezeka kwa asilimia 44.7 na kufikia shilingi trilioni 2.1 katika kipindi kilichoishia Aprili 2024, ikilinganishwa na shilingi trilioni 1.4 katika kipindi kilichoishia Aprili 2023.
Mnamo tarehe 16 Aprili 2024, Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) iliidhinisha Waraka wa Matarajio (Offer Document) na Mkataba wa Uendeshaji wa Mfuko wa Timiza. Idhini ilitolewa na CMSA baada ya Zan Securities Limited kukidhi matakwa ya Sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana Sura ya 79 ya Sheria za Tanzania na Miongozo ya Masoko ya Mitaji na Dhamana ya uanzishaji na uendeshaji wa Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja yaani Capital Markets and Securities (Collective Investment Schemes), Regulations 1997.
Napenda kutamka kuwa, Timiza Fund ni mfuko ambao umekidhi matakwa ya Sheria, Kanuni na Miongozo ya Uwekezaji wa Pamoja.
Timiza Fund ni mfuko unaoendeshwa na taasisi ya Zan Securities Limited ambaye ni Meneja wa Mfuko (Fund Manager) na Benki ya Mwanga Hakika ambaye ni Mtunza Dhamana wa Mfuko (Custodian).
Lengo kuu la Mfuko wa Timiza Fund ni kuhamasisha wawekezaji wadogo, wa kati, na wakubwa kuunganisha nguvu zao na kuwekeza kwa pamoja ili kunufaika na fursa zinazopatikana katika sekta ya fecha, hususan masoko ya mitaji. Aidha, malengo mahsusi ya Mfuko wa Timiza ni kuwawezesha watanzania wa kada mbalimbali, ikiwa ni pamoja na vijana, wanawake, makundi maalum, taasisi na mifuko ya hifadhi ya jamii kunufaika na uwekezaji katika masoko ya fedha; kujenga utamaduni wa kuweka akiba na kuwekeza miongoni mwa watanzania; na kuwawezesha wananchi kushiriki katika uchumi.
Kuanzishwa kwa Mfuko wa Timiza kunachangia utekelezaji wa mikakati ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi madhubuti wa Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuongeza wigo wa upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo na kuwezesha wananchi kiuchumi.
Katika hotuba yake kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 22 April 2021 Mhe. Rais, alianisha kuwa mojawapo ya vipaumbele vya Serikali ni kuendelea kuboresha Sera za Uchumi na Fedha. Utekelezaji wa azma hii umeakisiwa katika miongozo ya Serikali inayolenga kuimarisha upatikanaji wa rasilimali fedha kutoka vyanzo mbalimbali vya sekta ya umma na binafsi.
Miongozo hiyo ni pamoja na Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 2025/26 (FYDP III) wenye dhima ya Kujenga Uchumi Shindani kwa Maendeleo ya Watu; Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha 2020/21 2029/30; na Mpango wa Huduma Jumuishi za Fedha wenye lengo la kuongeza ushiriki wa wananchi kwenye sekta rasmi ya fedha ikiwa ni pamoja na masoko ya mitaji.
Katika juhudi za kuwezesha kufikia malengo ya kuanzishwa kwa Mfuko huu, Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), imeidhinisha kushusha kiwango cha chini cha ushiriki katika uwekezaji kwenye Mfuko huu kutoka Shilingi milioni moja (Tsh 1,000,000) hadi Shilingi elfu 10 (Tsh 10,000). Hatua hii ni muhimu kwani itawezesha ushiriki wa wawekezaji wa kada mbalimbali katika Mfuko huu, ikiwa ni pamoja na wananchi wenye vipato vya chini, vya kati na vikubwa.
Kwa mujibu wa Sera na Miongozo ya uwekezaji wa Mfuko wa Timiza, fedha zitakazopatikana kutoka kwa wawekezaji zitawekezwa katika masoko ya mitaji, ikiwa ni pamoja na kuwekeza katika Kampuni zilizoorodheshwa katika Soko la Hisa (Listed Equities), Hatifungani za Serikali (Treasury Bonds) na Hatifungani za Kampuni (Corporate Bonds). Lengo la uwekezaji wa aina hii ni kuufanya mfuko kuwa na ukwasi unaotosha ili kukidhi mahitaji ya fedha za wawekezaji pindi mahitaji yanapotokea.
Mhe. Exaud Kigahe (MB), Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mfuko wa Uwekezaji wa pamoja wa Timiza (Timiza Fund) wa Kampuni ya ZAN SECURITIES LIMITE leo Mei 27, 2024Uwekezaji katika Mfuko wa Timiza una manufaa mbalimbali katika ustawi wa jamii na maendeleo ya uchumi hapa nchini. Kwanza, unachangia katika utekelezaji wa Sera ya Serikali ya uwezeshaji wananchi kiuchumi kwa kuwezesha makundi mbalimbali ya jamii, ikiwa ni pamoja na watu wa kipato cha chini kuwekeza kwa pamoja katika dhamana za Serikali (Treasury Bonds) ambapo, katika hali ya kawaida wasingeweza kushiriki katika uwekezaji huo, kwani kima cha chini cha ushiriki ni Shilingi Milioni moja.
Pili, uwekezaji utakaofanywa na Mfuko huu katika hatifungani za Serikali utawezesha upatikanaji wa rasilimali fedha za kugharamia miradi ya maendeleo kama ambavyo ilivyoainishwa katika Mkakati wa Serikali wa njia mbadala za kugharamia miradi ya maendeleo yaani Alternative Project Financing (APF) Strategy.
Tatu, wawekezaji watalipwa gawio kutokana na faida za uwekezaji na wakati huo wakiwa ni sehemu ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kutokana na fedha za mfuko kuwekezwa katika hatifungani za Serikali. Faida nyingine ya kuwekeza katika Mfuko wa Timiza ni kuwa vipande vya uwekezaji vinaweza kutumika kama dhamana ili kuwezesha wawekezaji wa Mfuko kupata mikopo kutoka taasisi za fedha kwa ajili ya shughuli za maendeleo.
Aidha, mifuko ya uwekezaji wa pamoja inatoa anuwai ya uwekezaji kwa wananchi ambapo wawekezaji wanapata fursa ya fedha zao kuwekezwa katika maeneo na miradi mbalimbali na hivyo kuongeza wigo wa fursa.
Wadau wote wa masoko ya mitaji muendelea kushirikiana na Serikali katika kuongeza ushiriki wa wananchi katika fursa za kiuchumi na hivyo kufanikisha utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Kifedha na kuwezesha Serikali na Sekta Binafsi kupata rasilimali fedha za kugharamia shughuli mbalimbali za maendeleo, na hivyo kuchochea maendeleo ya kijamii na ukuaji wa uchumi hapa nchini






