Na John Walter-Mbulu
Wajasiriamali wilayani Mbulu Mkoani Manyara wamepatiwa Vifaranga 4,000 kama mtaji ili waweze kujikwamua kiuchumi na kuondokona na umaskini.
Akikabidhi vifaranga hivyo katika hafla iliyofanyika ukumbi wa walimu Mbulu mjini, Mbunge wa viti maalum mkoa wa Manyara Mheshimiwa Yustina Rahhi, amewataka wanawake walionufaika na Kuku hao wasitumie kwa kitoweo bali wafuge ili waweze kuinua vipato vyao na familia zao.
Aidha Rahhi amesema kuwa matarajio yake baada ya mwaka mmoja waliopata vifaranga hivyo waweze kubadilisha maisha yao.
"Watanufaika katika mambo mengi sana, watapata nyama, mayai ambayo watauza na Kuku wakizaliana watauza na kuongeza kipato"
Aidha amewataka wanufaika hao ambao wengi ni Wanawake, kwenda kutumia utaalam waliopewa kwenda kutoa elimu kwa wengine na kuleta tija kwa taifa kwa kujiongezea kipato chao na familia
Pia aliwashauri kutumia kuku hao kama chachu ya maendeleo ili kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kufika uchumi wa kati.
Madiwani wa viti maalum Halmashauri ya mji wa Mbulu waliohudhuria hafla ya kufunga Mafunzo hayo, wamesema "Wana Manyara wanabahati sana kwa hiyo watumie nafasi hiyo kwa ajili ya kujinufaisha, Mbunge anafanya kazi nzuri sana na wanampongeza,kina mama msimwangushe"
Kwa upande wake Mkufunzi kutoka taasisi ya Star Entrepreneur General Danford Kisaga kutoka mkoani Morogoro, amesema wajasiriamali zaidi ya 350 wamenufaika na mafunzo hayo ya vitendo na wameonesha shauku kubwa ya kwenda kujiajiri na kwamba wanachohitaji kwa sasa ni kuundwa vikundi mbalimbali pamoja na kupatiwa eneo maalum kwa ajili ya wajasiriamali.
Amesema Mafunzo hayo ni ya ujasiriamali kwa makundi mbalimbali Wanawake, Vijana na wenye ulemavu kwa lengo la kumkomboa mwananchi kiuchumi hasa katika maeneo ya usindikaji wa nafaka, mbogamboga, matunda, utengenezaji wa bidhaa mbalimbali za kemikali na ufugaji wa kuku.
"Wamejifunza kutengeza sabuni za Miche, batiki,karanga za mayai, keki, biskuti, utengenezaji wa tambi na Crips, na yote hayo ni ili kumuwezesha huyu mtanzania aweze kujiajiri " alisema Kisaga
Naye afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya wilaya ya Mbulu mjini Asha Tengu, amesema kwa sasa wapo katika mchakato wa kusajili vikundi vya wajasiriamali na kwamba waliopatiwa mafunzo hayo watapewa kipaumbele ikizingatiwa kwamba Halmashauri hiyo ni miongoni mwa zile kumi zilizochaguliwa kuanza majaribio ya kutoa mikopo ya asilimia 10 isiyo na riba.
Nao wajasiriamali watarajiwa wameahidi kwenda kujiajiri kufuatia Mafunzo waliyopatiwa.
Mbunge huyo alifadhili mafunzo ya siku sita kwa wajasiriamali ambao walijifunza jinsi ya kufuga kuku, kutengeneza keki, kutengeneza batiki pamoja na ufugaji wa kuku ili wafuge kwa ajili ya kujikimu kiuchumi na kuondokana na umaskini.
Kaulimbiu, Wajasiriamali Manyara tunasimama na Mheshimiwa Dr. Samia Suluhu Hassan kwenda uchumi wa kati.

