TGNP yawapika waandishi wa Habari ubobezi Habari za kijamii.



Na John Walter -Dar es Salaam

Wanawake  nchini wameshauriwa  kujitokeza kwa wingi na kugombea nafasi za uongozi kwenye ngazi za vijiji na vitongoji  katika  uchaguzi wa mwaka huu  wa Serikali za mitaa ili kuleta usawa na haki kwenye  maamuzi mbalimbali.

Mkurugenzi Mtendaji  wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP ), Lilian Liundi amesema  hayo , Jijini Dar es Salaam wakati akifungua mafunzo  ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia, uchaguzi na kilimo ikolojia.

Mafunzo  hayo yamehusisha  waandishi wa habari kutoka mikoa mitatu ya Manyara, Kilimanjaro na Morogoro  yatajikita katika maeneo matatu ambayo ni kujifunza mbinu za kuandika na kuripoti habari zenye athari chanya katika jamii , njia inayobadilisha mitazamo hasi na kuleta mabadiliko ya kweli.

Liundi amesema  TGNP pamoja na Pelum wanatekeleza mradi wa wanawake wa vijini kuleta mabadiliko (RWCC) kwa ufadhili wa Serikali ya Canada.

Amesema mradi unatekelezwa  katika mkoa wa Manyara kwenye  Wilaya ya Babati na Mbulu, Morogoro kwa wilaya ya  Gairo na halmashauri ya wilaya ya Morogoro na kwa mkoa wa Kilimanjaro  ni  katika wilaya ya Mwanga  na Same.

‘” Mradi huu unatekelezwa na TGNP pamoja Shirika la Usimamizi Shirikishi wa matumizi ya Ardhi Tanzania (PELUM TZ) na  ulianza  mwaka 2021 na utakamilika  mwaka 2026 “ amesema Liundi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao huo amesema mradi utawanufaisha wanawake wakulima wa vijijini  wapatao 5,364.

Pamoja na hayo amesema , ingawa  sheria ya uchaguzi wa serikali za mitaa  inalazimisha uwepo wa wanawake katika ngazi ya maamuzi, lakini bado ushiriki wao ni mdogo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mila kandamizi na hofu miongoni mwao.

“ Mafunzo hayo yamekuja kwenye wakati muafaka tukielekea kwenye uchaguzi wa Serikali za mtaa..hawa wanawake wakulima  wadogo wa vijijini tunafahamu wananafasi kubwa ya kushika nafasi za maamuzi katika uchaguzi huu” amesema  Liundi.

Liundi amesema  , waandishi wa habari wa vyombo vya ngazi ya jamii wanayo nafasi kubwa ya  kuhamasisha wanawake wakulima  wadogo wa vijijini kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi wa Serikali za mtaa.

Amesema kuwa  mafunzo hayo yatatoa fursa ya kuangalia hali halisi  na namna gani waandishi habari wanaweza kufanya kuhakikisha wanawake wanapata habari zaidi na kugombea nafasi hizo.

Kwa upande wa kilimo hai,  amesema kilimo hicho kinafaida ni cha asilia kwa sababu hakitumii dawa.

"Kilimo hiki kinatumia mbolea za asili na ni kilimo cha afya zaidi na wanawake wengi wa vijijini wamekuwa wakikitumia," amesema Liundi.

Amesema mradi huo utaangalia  namna wanawake wa vijijini ushiriki wao katika kilimo hai na hivyo  vyombo vya habari ngazi ya jamii vinaweza kuhamasisha zaidi ushiriki wao katika kilimo hicho na kukipa uzito kilimo hicho katika jamii.

Liundi amesema kuwa Serikali imeweza kutambua kwa kiwango fulani kuhusu kilimo hicho na kuna juhudi ambazo zimekuwa zikifanyika .

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items

Kilimo cha Bamia