TMA yatoa taarifa juu ya uwepo wa kimbunga ‘Hidaya’


Kufuatia taarifa iliyotolewa jana na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) juu ya kuwepo  kwa mgandamizo mdogo wa hewa katika Bahari ya Hindi mashariki mwa Pwani ya Mtwara, mgandamizo huo umeendelea kuimarika na kuwa kimbunga ‘Hidaya’ ambacho kina nguvu ya kati na umbali wa Kilomita 506 Pwani ya nchi ya Tanzania 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na TMA, imeeleza kuwa uwepo wa kimbunga hicho unatarajiwa kutawala na kuathiri mifumo ya hali ya hewa  hapa nchini ikiwa ni pamoja na kusababisha vipindi vya mvua kubwa na upepo mkali katika baadhi ya maeneo ya mkoa wa Mtwara, Lindi, Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Dar es Salaam,Tanga, Morogoro, Visiwa vya Unguja na Pemba na maeneo Jirani hususani Mei 3, 2024 kwa maeneo ya Pwani ya Kusini (Lindi na Mtwara).

TMA imesema kimbunga hicho kitasambaa katika maeneo mengine ya ukanda wa Pwani kuelekea Mei 4 hadi 6, 2024 na kwamba kutokana na hali hiyo wanatoa tahadhari kwa taasisi zinazojihusisha na masuala ya majanga kuendelea kufuatilia taarifa za kimbunga hicho.


Aidha TMA imewataka watu wanaofanya shughuli za usafirishaji baharini, wavuvi na wanaoishi maeneo ya Pwani ya Bahari ya Hindi kuendelea kuchukua tahadhari wakati kimbunga hicho kinatarajiwa kuingia usiku wa Mei 3, 2024.

Post a Comment

0 Comments