Wakuu wa mikoa na wilaya watakiwa kuanzisha operesheni za ulinziWaziri mkuu Kassim Majaliwa amewataka Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wahakikishe kila halmashauri inaanzisha operesheni maalum za ulinzi kwa watu wenye ualbino.
 
“Operesheni hizi zihusishe vikosi vya usalama ili kuhakikisha ulinzi wa watu wenye ualbino dhidi ya mashambulizi na vitisho hii ni kwa sababu katika kuzuia unyanyasaji na mauaji ya watu wenye ualbino, Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa zinawajibika katika usimamizi, ulinzi na utoaji wa huduma kwa watu wenye ualbino,” amesema.
 
Ametoa wito huo leo (Alhamisi, Juni 20, 2024) wakati akitoa taarifa kuhusu kupinga ukatili dhidi ya watu wenye ualbino wakati wa kipindi cha maswali ya Papo Kwa Papo kwa Waziri Mkuu, Bungeni, jijini Dodoma.
 
Waziri Mkuu amezitaka Mamlaka za Mikoa na Wilaya zihamasishe ushiriki wa jamii katika kuhakikisha ulinzi na haki za watu wenye ualbino kwani vitendo vya mauaji ya albino vinahusisha mtandao wa watu na siyo mtu mmoja mmoja tu.
 
Amesema Serikali tayari imeshajenga mifumo thabiti ya udhibiti na suala lililobaki ni ushiriki wa makundi yote ya jamii katika kuhakikisha vitendo hivyo viovu vinakomeshwa hapa nchini. “Kwa kutambua jukumu tulilonalo kama Taifa, nitumie nafasi hii kuyataka makundi na taasisi mbalimbali katika jamii kuendelea kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya vitendo hivyo vya ukatili.
 
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewaomba viongozi wa dini waendelee kukemea  kukemea maovu yanayotendeka nchini hususan mauaji kwa watu wenye ualbino kwani kuwepo kwa matukio hayo kunaonesha upotofu wa maadili na kukosa hofu ya Mungu.
 
“Nitumie nafasi hii kuwaomba viongozi wetu wa dini tuungane pamoja kupambana na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia hata kidogo. Ninawasihi watumie majukwaa yao ya ibada kuwahubiria waumini wao waachane na vitendo hivyo vya ukatili ambavyo hata Mwenyezi Mungu anavikataza. Watu wenye ualbino wana haki ya kuishi kama walivyo watu wengine,” amesisitiza.
 
Waziri Mkuu amesema waganga wa jadi nchini kote wanapaswa kushiriki kikamilifu katika kampeni za kupinga mauaji ya watu wenye ualbino. “Wakati umefika kwenu nyote kushirikiana na Serikali katika kutokomeza imani potofu zinazochangia mauaji haya. Ninawasihi sana elezeni wazi kwamba hakuna tiba wala mafanikio yanayoweza kupatikana kwa kutumia viungo vya watu wenye ualbino.”
 
Pia amelitaka Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala lifanye usajili wa waganga wa jadi na vituo vyao sambamba na aina ya huduma wanayoitoa kwa wateja wao ili kuweza kudhibiti huduma holela isiyofuata misingi ya utu na haki za binadamu.
 
Mbali na hao, amewataka viongozi wa kimila kutoka kila kona ya Tanzania washiriki kikamilifu katika kukemea na kupinga mauaji ya watu wenye ualbino. “Ninawaomba viongozi wetu wa kimila wakiwemo machifu washirikiane na Serikali kwa kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama pindi wanapopata fununu za mipango au vitendo vya mauaji ya watu wenye ualbino katika maeneo wanayoishi.”
 
Ili kuhakikisha matukio ya aina hiyo hayatokei, Waziri Mkuu amelielekeza Jeshi la Polisi lichukue hatua za haraka pindi linapopata fununu ya uwepo wa njama za utekaji na mauaji ya watu wenye ualbino.
 
Pia ametaka liendelee kufanya operesheni ya kuwakamata wote waliotajwa na watakaotajwa kuhusika kwenye matukio ya aina hii ili kuua mtandao mzima wa wahalifu. “Polisi jamii ishirikishwe kikamilifu ili kupata taarifa zote muhimu katika maeneo husika na watoa taarifa wote walindwe ipasavyo,” amesisitiza.
 
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema lengo la Serikali ni kuwalinda wananchi walioathirika kwa kuwa wanahitaji kuwekwa mahali salama kwa kuwa bado wanakuwa wana hofu kutokana na madhila yaliyowafika.
 
“Sera yetu ya Serikali ni kuwalinda wote wenye ulemavu wa aina yoyote ili washiriki shughuli za maendeleo huku tukihakikisha wanakuwa salama. Malengo yetu ni kutoa uhakika wa maisha yao wakati wote.
 
“Bado tunaendelea kutafuta njia mbadala ikiwemo kuwachanganya ili wasijione wametengwa. Tumeanza kuwachanganya katika shule za msingi na sekondari ili nao washiriki pamoja kwenye shughulimbaliza kijamii na michezo bila kujali ulemavu wao.”
 
Alikuwa akijibu swali la Rashid Shangazi (Mbunge wa Mlalo) ambaye alimtaka Waziri Mkuu aeleze ni kwa nini Serikali inapanga kuwaweka waathirika kwenye kambi ilhali ni kinyume na haki ya kuwa huru kama ilivyoelezwa kwenye ibara ya 15(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Post a Comment

0 Comments