Na John Walter -Babati
Mkaguzi Msaidizi wa Polisi na Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Babati, Fatuma Silaa, amesema kuwa katika kipindi cha Januari hadi Machi 2025, jumla ya matukio 68 ya ukatili wa kijinsia yameripotiwa wilayani humo, huku watoto wakihusishwa katika matukio 36 na watu wazima 32.
Akizungumza mbele ya kikao cha wadau wa mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia kilichofanyika mjini Babati, Fatuma Silaa ameeleza kuwa miongoni mwa matukio hayo ni pamoja na kesi 19 za ubakaji, kesi 4 za kujaribu kubaka, kesi 12 za kulawiti, kesi 7 za kumpa mwanafunzi mimba, na kesi 3 za kutorosha wanafunzi.
Amesema licha ya changamoto zilizopo, huduma ya Mobile Station iliyozinduliwa na Dawati la Jinsia imekuwa msaada mkubwa katika kuwafikia waathirika, kupokea taarifa na kutoa msaada wa kisheria na kisaikolojia kwa wahanga wa ukatili.
Katika kikao hicho, watendaji wa kata, mitaa, vijiji, wanasheria wa Halmashauri, Jeshi la Magereza, Polisi na wadau mbalimbali wa haki za binadamu wamekutana kujadili mikakati ya kutokomeza vitendo vya ukatili katika Wilaya ya Babati.
Wadau hao wameazimia kushirikiana kwa karibu na jamii kupitia mfumo wa kuripoti matukio ya ukatili kwa kutumia fomu maalum kuanzia ngazi ya kata, mitaa hadi vijiji, pamoja na kuendelea kutoa elimu na kuwajengea uwezo watendaji wa ngazi ya msingi kuhusu sheria na haki za waathirika wa ukatili.


Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalum Halmashauri ya Mji wa Babati, Ali Mwinyikombo, amesema:
“Tunahitaji mshikamano wa kweli kutoka kwa kila mdau, tukitumia mfumo huu wa kuripoti matukio ya ukatili kwa ufanisi na kutoa elimu kwa jamii, tunaweza kuokoa maisha na mustakabali wa kizazi chetu.”
Wadau wameahidi kuendelea kushirikiana katika kuimarisha ulinzi wa watoto na wanawake kwa kuweka mazingira salama na yenye haki kwa wote.
0 Comments