F Sillo atangaza neema Kiru, ujenzi wa kituo cha afya kuanza muda wowote. | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Sillo atangaza neema Kiru, ujenzi wa kituo cha afya kuanza muda wowote.



Na John Walter -Babati 

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini, Mheshimiwa Daniel Sillo, ametangaza habari njema kwa wakazi wa Kata ya Kiru baada ya kuthibitisha kuwa serikali imeanza rasmi maandalizi ya ujenzi wa Kituo cha Afya katika kata hiyo.

Kupitia ujumbe aliouweka kwenye mitandao ya kijamii, Mheshimiwa Sillo amesema kuwa tayari serikali imeshatoa kiasi cha shilingi milioni 250 kama awamu ya kwanza ya fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kituo hicho muhimu cha afya. 

Ameeleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha huduma za afya zinawafikia wananchi kwa ukaribu na kwa ubora unaostahili.

Hapo awali, walikuwa wakitumia zahanati chakavu ambayo haina vifaa wala huduma za kutosha, hali iliyokuwa ikihatarisha maisha yao, hasa kwa akinamama wajawazito na watoto.

Ripoti ya Walter Habari iliangazia kilio cha wananchi hao wakiiomba serikali kuwapatia kituo cha afya cha kisasa ili kuondokana na adha ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya.

Hatua hii ni ishara ya dhamira ya serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ya kupeleka maendeleo vijijini na kuboresha huduma muhimu kwa wananchi.

Kwa sasa, wakazi wa Kiru wanasubiri kwa matumaini utekelezaji wa ujenzi huo uanze mara moja ili waweze kunufaika na huduma bora za afya kwa ukaribu zaidi.

Post a Comment

0 Comments