F Kafulila, Mukandala, Tibaijuka kwenye mjadala wa Ubia UDSM kesho | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Kafulila, Mukandala, Tibaijuka kwenye mjadala wa Ubia UDSM kesho


KITUO cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC) kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti na Elimu kwa Demokrasia Tanzania (REDET) kinatarajia kufanya kongamano muhimu kesho, Mei 27, 2025, katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwa lengo la kujadili nafasi ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam leo Mei 26, 2025 Mkurugenzi Mtendaji wa PPPC, Bw. David Kafulila, amesema `kongamano hilo litafanyika katika jengo la Ukumbi wa Maktaba Mpya ya UDSM na litawakutanisha wasomi, watendaji wakuu wa mashirika, viongozi wa kibiashara pamoja na wadau mbalimbali wa sekta binafsi.

"Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi una nafasi kubwa katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa uwezo wake wa kusaidia kujenga ustahimilivu dhidi ya misukosuko ya nje na changamoto za kifedha za umma," alisema Kafulila.

Ameongeza kuwa serikali imeweka dhamira thabiti ya kuleta maendeleo makubwa kupitia dira hiyo, ambapo sekta binafsi imetambuliwa kama mhimili muhimu wa ukuaji wa uchumi wa nchi.

Pia alisisitiza umuhimu wa Tanzania kujitegemea kiuchumi kwa kupanua vyanzo vya kifedha hasa katika muktadha wa mabadiliko ya kimataifa kwenye mifumo ya ufadhili wa maendeleo. Kongamano hilo litaangazia kwa kina masuala kama vile masoko ya mitaji ya kimataifa, uhamasishaji wa kifedha, fursa na changamoto zinazohusiana na PPPs.

Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Fedha, Tanzania ina miradi 80 ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi inayotekelezwa katika hatua mbalimbali, ikiwa ni ishara ya dhamira ya serikali kuimarisha ushirikiano huo.

Serikali imefanya mageuzi mbalimbali ya kisheria na ya kikanuni ili kurahisisha mazingira ya uwekezaji na kuhamasisha ushiriki wa Sekta Binafsi katika miradi ya kimkakati ya kitaifa.

Kongamano hilo linatarajiwa kutoa mchango muhimu wa kitaalamu kutoka kwa wanazuoni wa UDSM na kuchochea mijadala yenye tija kuhusu namna bora ya kutumia PPPs kama chachu ya maendeleo ya Taifa kuelekea mwaka 2050.


Profesa Mukandala alitumia fursa hiyo kuwaomba wananchi kuhudhuria kongamano hilo la wazi ili waweze kushiriki kwenye mjadala kuhusu dhana ya PPP na nafasi yake kwenye kutekeleza Dira ya Taifa 2050.

Post a Comment

0 Comments