F Madaktari 48 Kutoa Huduma za Kibingwa kwa Siku Sita Mkoani Manyara | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Madaktari 48 Kutoa Huduma za Kibingwa kwa Siku Sita Mkoani Manyara



Na John Walter -Manyara, 
Jumla ya madaktari bingwa 48 pamoja na wauguzi wabobezi wamewasili mkoani Manyara kwa ajili ya kutoa huduma za kibingwa kwa siku sita mfululizo katika halmashauri zote saba za mkoa huo, ikiwa ni sehemu ya jitihada za serikali kusogeza huduma bora karibu na wananchi.

Akizungumza wakati wa mapokezi ya timu hiyo ya wataalamu, Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Michael Semindu, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara, alisema kuwa huduma hizo ni utekelezaji wa maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya bila usumbufu wa kusafiri umbali mrefu au kutumia gharama kubwa.

“Huu ni mwendelezo wa juhudi za serikali katika kuboresha sekta ya afya. Wananchi watapata huduma za kibingwa wakiwa karibu na makazi yao, jambo litakalosaidia kupunguza gharama na muda wa kusubiri,” alisema Semindu.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Dkt. Henry Method, alibainisha kuwa wananchi watakaofika kupata huduma hawatatozwa gharama za ziada, bali watalipa viwango vya kawaida kama ilivyo kwenye vituo vyao vya afya.

Mratibu wa mpango huo kutoka Wizara ya Afya kwa upande wa Mkoa wa Manyara, Paskalina Henry, alisema mbali na kutoa huduma kwa wananchi, madaktari hao pia watajenga uwezo wa wataalamu wa afya waliopo katika vituo vya kutolea huduma, ili huduma hizo ziendelee kutolewa hata baada ya madaktari hao kuondoka.

“Nitoe wito kwa wananchi wote wa Manyara kujitokeza kwa wingi kupata huduma hizi muhimu. Ni fursa adimu ya kuonana na madaktari bingwa bila kwenda hospitali kubwa,” alisema Paskalina.

Akizungumza kwa niaba ya madaktari wenzake, Dkt. Michael Haule aliahidi kuwa timu hiyo imejipanga kikamilifu kuhakikisha wananchi wote wanaofika wanapata huduma bora na kwa wakati.

Huduma hizo zinatarajiwa kutolewa katika halmashauri za Mbulu Mji, Mbulu DC, Babati Mji, Babati DC, Hanang’, Kiteto na Simanjiro.


Post a Comment

0 Comments