Baadhi ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma UDOM, walionufaika na mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa JKT kwa mujibu wa Sheria ambayo hupewa wahitimu wa kidato cha sita kabla ya kujiunga na Vyuo Vikuu wamesema mafunzo hayo ni msaada mkubwa kwani yanasaidia kuwajenga vijana katika hali ya uzalendo na kujitegemea.
Hivyo wamewataka vijana na wazazi kupuuza maneno ya baadhi ya watu wanaodai kuwa mafunzo hayo hayana umuhimu au manyanyaso kwa wanafunzi hasa Watoto wa kike.
Wakizungumza na Muungwana Blog Chuoni hapo wanafunzi hao wamesema mafunzo hayo yamewasaidia sana na wamefaidika kwa kujengewa uwezo wa kujiamini, kujitegemea, uzalendo na uzalishaji mali kwa kuwa wamefundishwa kilimo na mifugo ambayo inawasaidia katika maisha ya kila siku.
"Mafunzo haya yana umuhimu mkubwa sana kwa vijana kwa sababu yanawajenga kiafya,kiakili lakini pia yanawafundisha vitu mbalimbali vya kujitegemea ikiwemo ujasiriamali wa vitu mbalimbali, amesema Julius mtugonza".
Kutokana na hilo amewataka baadhi ya wazazi kuacha dhana potofu ya kudhani kwamba mafunzo hayo yanawapa vijana wao mateso badala yake wahimize vijana kwenda kujiunga na mafunzo hayo kwa mujibu wa sheria.
Kwa upande wake Katibu wa fedha katika serikali ya wanafunzi chuo Kikuu cha UDOM bw. Frolentino Kamiguzi amesema suala la kuongoza wanafunzi wenzio sio kitu kidogo kama hujapita kwenye mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria kwa sababu yanasaidia kujengea uwezo vijana katika kutekeleza vitu mbalimbali.
"Mfano mzuri unaniona hapa chuoni kwetu UDOM viongozi tunavyoiongoza vizuri serikali ya Chuo ukiuliza hawa wote wamepitia mafunzo ya JKT kwa mujibu wa Sheria sababu tunaongoza kundi la vijana wenye umri balehe kwahiyo mafunzo yale yanatusaidia sana,"amesema Frolence.
Kutokana na hilo amesema vijana wasikubali kupotoshwa na maneno ya mitandaoni kuhusu ushiriki wa mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria badala yake wajiunge kwenda kujifunza Uzalendo,Nidhamu pamoja na ujasiriamali wa aina mbalimbali.
Amesema wengi wa vijana waliopita katika mafunzo hayo ukiwafuatilia wako vizuri kwenye nidhamu,uzalendo na uongozi pia kutokana na kupikwa vizuri kupitia mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa JKT Meja Jenerali Rajab Mabele mafunzo hayo yamewekwa kwa lengo la kuwajenga vijana Uzalendo, ukakamavu, nidhamu, umoja wa kitaifa, stadi za kazi, stadi za maisha na utayari wa kulitumikia taifa.
Hivi karibuni JKT limetangaza kuwaita vijana waliohitimu kidato cha sita kujiunga kwenye makambi yaliyo katika maeneo mbalimbali hapa nchini kuanzia mei 28 hadi Juni 8, 2025 ili kupata mafunzo hayo na orodha ya majina na mahali walipopangiwa inapatikana kupitia www.jkt.mil.tz .
0 Comments