Na John Walter-Manyara
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Babati (BAWASA) na
Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) mkoa wa Manyara
zimekubaliana kushirikiana kwa karibu katika utekelezaji wa miradi ya maji kwa
lengo la kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2025–2030.
Makubaliano hayo yamefikiwa katika kikao kazi cha sekta ya
maji kilichofanyika mjini Babati, kikibeba kauli mbiu isemayo “Pamoja
tujenge huduma bora za maji kwa maendeleo ya mkoa wa Manyara.”
Kikao hicho kimewakutanisha wakuu wa taasisi hizo
wakiongozwa na Meneja wa RUWASA Mkoa wa Manyara, Mhandisi James Kionaumela,
pamoja na Mkurugenzi wa BAWASA, Mhandisi Iddy Msuya, ambapo wamejadili mikakati
ya kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika maeneo ya
mijini na vijijini mkoani humo.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhandisi Kionaumela amesema
ushirikiano kati ya RUWASA na BAWASA utaongeza ufanisi, kupunguza changamoto za
utekelezaji wa miradi na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora ya maji kwa
wakati.
Kwa upande wake, Mhandisi Msuya amesema kuwa hadi sasa
huduma ya maji katika mji wa Babati imefikia asilimia 85, huku kiwango cha
upatikanaji wa maji kwa mkoa mzima wa Manyara kikiwa ni asilimia 75, hali
inayotoa msingi mzuri wa kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi mipya na ya
maboresho.
Mkuu wa Maabara ya maji mkoa wa Manyara Nicolaus Germanus,
amesema hali ya ubora wa maji katika mkoa wa Manyara inaridhisha.
Naye Mhandisi wa maji kutoka Bonde la maji, bonde la kati katika ofisi ya Babati Denis Gunze, amesema wameweka mikakati ya kuhakisha wanafanya utafiti juu ya upatikanaji wa maji sehemu yenye maji.
Viongozi hao wamesisitiza kuwa ushirikiano huo ni sehemu ya
utekelezaji wa Ilani ya CCM, sambamba na adhma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma
ya maji safi na salama kwa uhakika na hivyo kuwapatia tabasamu wananchi.
Kwa mujibu wa Ilani ya CCM 2025–2030, mkoa wa Manyara
unatarajiwa kufikia kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji kwa asilimia 99
ifikapo mwaka 2030, lengo ambalo BAWASA na RUWASA wameahidi kulifanyia kazi kwa
nguvu, ubunifu na mshikamano.
0 Maoni